WANAHABARI TACOEJ WAKABIDHIWA CHETI CHA USAJILI
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Said Mtanda amekabidhi rasmi cheti cha usajili wa Chama cha Waandishi wa Habari za Pamba na Mazingira (Tanzania Cotton and Environmental Journalists-TACOEJ).
Mtanda alikabidhi cheti hicho Jumanne Novemba 03, 2026 ofisini kwake alipotembelewa na viongozi wa chama hicho na kuwaahidi ushirikiano katika kuhamasisha kilimo chenye tija.
Alisema atahakikisha anajifunza kwa haraka kuhusu Kilimo cha Pamba na kwamba atashirikiana na waandishi wa habari za pamba kuhamasisha wakulima wa pamba kuongeza tija ili kukuza Uchumi wa wakulima wa pamba.
"Pamba ni uti wa mgongo wa uchumi wa Mkoa wa Simiyu, zao hili lina changamoto nyingi sana na mimi ninatakiwa kujifunza haraka nijue changamoto hizo" alisema Mtanda na kuongeza;
"Tunayo maagizo ya Serikali kufanya vikao vya wadau, ninyi mnataka kufanya kongamano, mimi naona ni tofauti...ninyi tunatakiwa tushirikiane na mamlaka zetu kuandaa kikao cha wadau kwa ajili ya zao la pamba na ninyi mtatumia kalamu zenu kiuandishi kufikisha ujumbe mkiwa ni sehemu ya wadau wa pamba ili yale tuliyokubaliana tuyatolee elimu kwa umma" alisema.
Alisema lengo ni kuongeza uzalishaji wa pamba kutoka tani 133,000 na kufikia tani 200,000... hivyo ni lazima kufanya jitihada kwa kushirikiana na waandishi wa habari za pamba na mazingira ili jamii na umma ujue uchumi wa Simiyu unategemea zao la pamba.



No comments: