LIVE STREAM ADS

Header Ads

TANESCO, REA WATAKIWA KUUNGANISHIA WANANCHI UMEME KWA WAKATI

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba ameagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kuhakikisha ndani ya siku tatu wanawaunganishia umeme wateja baada ya kufanya malipo.

Makamba ametoa agizo hilo Jumatatu Februari 23, 2026 wakati akiwasha umeme katika Kitongoji cha Bugofuma, Kijiji cha Ngeleka Kata ya Fela, Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, kilichofikishiwa umeme kupitia mradi unaotekelezwa na TANESCO kwa shilingi milioni 174 katika Vitongoji 121 wilayani Misungwi.

"Sisi Wizara ya Nishati tumeshawaelekeza REA na TANESCO kuhakikisha  uwa katika miradi ya umeme vitongojini inayoendelea mtu akilipia leo, zisipite siku tatu hadi nne awe amewekewa umeme. Na hapa Bugofuma tumeona TANESCO wametekeleza agizo hili kwani kati ya wananchi wa awali 35 waliolipia huduma jana, tayari wananchi 22 wameunganishiwa umeme" amesema Makamba.

Ameeleza kuwa kasi ya uunganishiaji wateja umeme ni utekelezaji pia wa Mpango Mahususi wa Taifa wa Nishati (National Energy Compact 2025–2030), unaolenga kukuza upatikanaji wa umeme kufikia asilimia 100 katika maeneo ya vijijini na mijini, pamoja na kuongeza uunganishwaji wa umeme kwa kaya hadi kufikia asilimia 75.

Makamba pia amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi thabiti na wenye kujali utu, ukiwa na azma ya kuhakikisha vitongoji vyote nchini vinapata huduma ya umeme ya uhakika na nafuu ifikapo mwaka 2030.

Ameongeza kuwa wateja wote katika kitongoji hicho watafungiwa mita janja (smart meters) zitakazowawezesha kununua umeme wakiwa popote bila ya kuhitajika kuingiza namba za token kama ilivyokuwa awali.

Pia Makamba ameziagiza TANESCO na REA kufikisha nishati ya umeme kwa taasisi zinazotoa huduma kama vile vituo vya afya, shule, vituo vya polisi na masoko na kuendelea kuchochea matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Pia ametoa wito kwa Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kuboresha maeneo ya masoko na stendi kwa kuwa na maeneo maalumu ya kupikia ili kuwezesha uwekaji wa miundombinu ya kisasa ya nishati safi ya kupikia.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Misungwi, Silvery Salvatory amepongeza kasi ya Wizara ya Nishati katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya nishati, ikiwemo ya umeme vitongojini.

Pia ameshukuru Serikali kwa Jimbo la Misungwi kutengewa vitongoji 121 kupitia mradi uliosainiwa hivi karibuni wa upelekaji umeme katika vitongoji 9,009 nchini.

Naye Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati (Umeme na Nishati Jadidifu), Mhandisi Edson Ngabo amesema Wizara inaendelea kutekeleza miradi ya umeme vitongojini katika maeneo mbalimbali nchini.

Pia amewashauri wananchi kujiunga na huduma ya umeme kabla mradi haujafika mwisho na wautumie umeme huo kwa shughuli za kiuchumi. Wilaya ya Misungwi ina vitongoji 724, ambapo vitongoji vyenye umeme ni 323, huku kazi ya usambazaji umeme katika vitongoji vilivyosalia ikiendelea. 
Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba akizungumza wakati wa hafla ya kuwasha umeme katika Kitongoji cha Bugofuma, Misungwi mkoani Mwanza. 
Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba (wa tatu kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Johari Samizi (wa pili kulia) wakicheza ngoma ya asili ya kabila la wasukuma wakati wa hafla ya kuwasha umeme katika Kitongoji cha Bugofuma wilayani Misungwi.
Wakati wa Bugofuma wilayani Misungwi wakifuatilia hafla ya uwashaji umeme.
Burudani ya kucheza na nyoka.
TAZAMA VIDEO HAPA CHINI

No comments:

Powered by Blogger.