LIVE STREAM ADS

Header Ads

KSG YAVUTIWA NA MAFUNZO YA TPSC DAR ES SALAAM

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com

Dar es Salaam- Mei 5, 2026

Mkurugenzi Mkuu wa Shule ya Serikali Kenya (KSG), Prof. Nura Mohamed na ujumbe wake   wametembelea Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania leo, Mei 5, 2026, jijini Dar es Salaam.
Ziara hiyo ni sehemu ya kuanza kwa utekelezaji wa mkataba wa ushirikiano uliosainiwa Ikulu, Mei 4, 2026, mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Kenya, Mhe. Dkt. William Ruto.

Katika kikao cha pamoja na Menejimenti ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, chini ya Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu, Dkt. Ernest Mabonesho, wamejadiliana kwa kina kuhusu mikakati ya kuanza utekelezaji wa makubaliano hayo, huku lengo likiwa ni kuboresha utendaji wa utumishi wa umma kwa kuwajengea uwezo watumishi na Tafiti Tumizi.
Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu, Dkt. Ernest Mabonesho amesema  kuwa, ushirikiano kati KSG na Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania  (TPSC) unalenga kuleta maendeleo makubwa na ufanisi zaidi katika sekta ya utumishi wa umma, kwa kujenga uwezo wa watumishi kupitia mafunzo na tafiti.

 Aidha, alisisitiza kuwa, kutokana na uzoefu wa zaidi ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa KSG, ni fursa adhimu kwa TPSC kujifunza na kupata uzoefu wa kuboresha utumishi wa umma nchini Tanzania, ili kujenga utumishi wa umma imara.

Dkt. Mabonesho ameongeza kuwa, mashirikiano pia yanalenga kujenga utumishi wa umma wenye tija, wenye kuzingatia matokeo, na kuleta maendeleo chanya kwa wananchi wa Tanzania, Kenya, na jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla.
Kwa upande wake, Prof. Nura Mohamed alieleza kuwa, utekelezaji wa mkataba huo utaleta maendeleo makubwa kwa pande zote mbili, kwa kuimarisha mafunzo yanayozingatia ubora na haki za wananchi.

 Prof. Mohamed amesisitiza  kuwa, ushirikiano huo utahusisha pia kufanya tafiti za pamoja kuhusu kuboresha sera na huduma zinazohudumia jamii, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, ambazo ni haki yao ya msingi.

Ziara hiyo pia iliwapa nafasi ujumbe kutoka KSG kutembelea Makao Makuu ya Chuo yaliyopo Barabara ya Bibi Titi, Kampasi ya Dar es Salaam iliyopo Magogoni, na Kituo cha Mafunzo kwa njia ya Mtandao, ambapo walijionea mazingira ya mafunzo na shughuli zinazofanywa na chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania.




No comments:

Powered by Blogger.