LIVE STREAM ADS

Header Ads

MWANZA WAPANDA MITI KUELEKEA MAADHIMISHO YA SIKU YA ZIWA VICTORIA

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Wananchi na viongozi mbalimbali wameshiriki zoezi la upandaji miti katika chanzo cha maji Butimba jijini Mwanza, ikiwa ni sehemu ya shughuli za utunzaji na uhifadhi wa mazingira kuelekea kwenye maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Ziwa Victoria.

Zoezi hilo la upandaji miti Jumatatu Mei 18, 2026 likiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda  ambaye amesisitiza kuwa uhifadhi wa Ziwa Victoria ni muhimu kutokana na mchango wake mkubwa katika shughuli za kiuchumi na kijamii ikiwemo uvuvi, biashara, usafiri na upatikanaji wa maji kwa wananchi.

Amesema zaidi ya watu milioni 40 wanategemea ziwa hilo katika kujipatia kipato na kuendesha shughuli mbalimbali za maendeleo, hivyo ipo haja ya kuweka mikakati madhubuti ya kulinda mazingira na vyanzo vya maji ili kuhakikisha rasilimali hiyo inaendelea kuwa salama kwa kizazi cha sasa na kijacho.

“Hatupandi miti kwa ajili yetu pekee bali kwa ajili ya vizazi vijavyo ili vinufaike kama sisi tunavyonufaika kupitia waliopanda miti zamani” amesema Mtanda akitoa rai pia kwa wananchi kuwa na utamaduni wa kupanda miti katika maeneo yao ili kusaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Pia amewakaribisha wananchi kushiriki maadhimisho ya Siku ya Ziwa Victoria kuanzia Mei 18- 21, 2026 katika uwanja wa Nyamhongolo ambapo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha Siku ya Ziwa Victoria, Mei 21, 2026.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Rose Ambrose amesema Serikali inaendelea kuimarisha mradi wa maji Butimba unaohudumia zaidi ya wananchi 450,000 ili kufikia lengo la kuhudumia wananchi 800,000 ambapo kwa sasa unazalisha lita milioni 48 kwa siku huku lengo likiwa kuzalisha lita milioni 96 kwa siku.

Amebainisha pia mkakati wa wizara hiyo wa kupanda miti 10,000 ambayo ni rafiki wa maji katika maeneo mbalimbali ikiwemo eneo la mradi wa maji Butimba ambapo hadi sasa miti zaidi ya 6,500 tayari imepandwa na kwamba zoezi la upandaji miti leo ni sehemu ya uzinduzi wa zoezi la kupanda miti 5,000.

Zoezi la upandaji miti katika chanzo cha maji Butimba jijini Mwanza limeratibiwa na Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB), ikiwa ni mwanzo wa shughuli za maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Ziwa Victoria inayofanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania, Mei 21, 2026 yenye kauli mbiu isemayo "Maji Yetu, Mstakabali Wetu: Tuungane kwa Eendelevu wa Bonde la Ziwa Victoria".

Maadhimisho ya Siku ya Ziwa Victoria yalianzishwa kufuatia azimio la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kupitia Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) katika kikaokilichoketi mwakauliopita 2025 nchini Kenya, lengo likiwa ni kuhamasisha uhifadhi wa ziwa hilo kwa matumizi endelevu kiuchumi na kijamii.
Na George Binagi, Mwanza
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Amina Makilagi akizungumza wakati wa zoezi la kupanda miti katika chanzo cha maji Butimba ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Ziwa Victoria yaliyoanza Mei 18- 21, 2026 jijini Mwanza.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akizungumza wakati wa zoezi la kupanda miti katika chanzo cha maji Butimba ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Ziwa Victoria.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Rose Ambrose akizungumza wakati wa zoezi la kupanda miti katika chanzo cha maji Butimba ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Ziwa Victoria.
Katibu Mtendaji Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria, Masinde Bwire akizungumza kwenye zoezi la upandaji miti katika chanzo cha maji Butimba jijini Mwanza.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda akiongoza zoezi la upandaji miti katika chanzo cha maji Butimba.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Rose Ambrose akipanda mche katika chanzo cha maji Butimba jijini Mwanza.
Mwenyekiti Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, Emmanuel Lugomela akipanda mche katika chanzo cha maji Butimba jijini Mwanza.
Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria, Dkt. Renatus Shinhu akipata mti katika chanzo cha maji Butimba jijini Mwanza.
Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi akipanda mti katika eneo la chanzo cha maji Butimba jijini Mwanza ikiwa ni sehemu ya shughuli zinazofanyika kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Kwanza ya Siku ya Ziwa Victoria, Mei 21, 2026.

No comments:

Powered by Blogger.