MRADI WA TASNIA YA MAZIWA NA MABADILIKO YA TABIANCHI (C-SDTP) WALETA HAMASA YA UZALISHAJI WA MAZIWA UNAOZINGATIA MABADILIKO YA TABIANCHI
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mratibu wa Taifa wa Mradi wa Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi (C-SDTP) Dkt. Lazaro Kapella ameeleza,"C-SDTP, chini ya mwongozo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, inaendelea kusaidia wazalishaji wadogo wa maziwa kwa kuimarisha ushiriki wao katika mnyororo wa thamani wa maziwa, kuongeza mapato ya kaya, kuboresha usalama wa chakula na lishe, na kupunguza athari za kimazingira zitokanazo na mifumo ya uzalishaji wa maziwa".
Sehemu ya Wafanyakazi wa Mradi wa C-SDTP wakiwa kwenye banda la maonesho wakati wa Wiki ya Maziwa Kitaifa Mkoani Iringa.
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia mradi wa Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi (C-SDTP), kwa kushirikiana na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), imeungana na wadau wengine wa kitaifa maadhimisho ya Wiki ya Maziwa kitaifa katika viwanja vya Mwembe Togwa, mkoani Iringa kuanzia 25 Mei hadi 1 Juni 2026 kwa lengo la kuhamasisha ufugaji wa ng'ombe na uzalishaji wa maziwa unaozingatia mabadiliko ya tabianchi.
Maadhimisho hayo yameandaliwa na Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), na kuwaleta pamoja wadau muhimu katika mnyororo wa thamani wa maziwa, ikiwa ni pamoja na wakulima, wachakataji, taasisi za Serikali, taasisi za kifedha, washirika wa maendeleo,na maafisa wa Serikali ili kujadili fursa za uwekezaji, viwango vya ubora, na teknolojia bunifu kwa maendeleo ya sekta ya maziwa.
Katika maadhimisho haya, mradi wa C-SDTP unaonesha jitihada zake katika kufanya mabadiliko katika sekta ya maziwa kwa kuimarisha uzalishaji maziwa kwa wakulima wadogo katika mikoa nane inayotekeleza mradi huu ikiwemo mikoa ya Iringa, Mbeya, Morogoro, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, na Pwani; pamoja na Zanzibar (Pemba na Unguja).
Mratibu wa Taifa wa Mradi wa Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi (C-SDTP) Dkt. Lazaro Kapella ameeleza,"C-SDTP, chini ya mwongozo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, inaendelea kusaidia wazalishaji wadogo wa maziwa kwa kuimarisha ushiriki wao katika mnyororo wa thamani wa maziwa, kuongeza mapato ya kaya, kuboresha usalama wa chakula na lishe, na kupunguza athari za kimazingira zitokanazo na mifumo ya uzalishaji wa maziwa".
Katika maadhimisho haya ya Wiki ya Maziwa, mradi wa C-SDTP unaongeza uelewa wa umma kuhusu umuhimu wa unywaji wa maziwa na kukuza mbinu bora katika ufugaji wa ng’ombe, zikiwemo ufugaji wa mbari bora za ng'ombe wa maziwa, upandikizaji wa mbegu za ng’ombe (Artificial Insemination), uzalishaji wa malisho, huduma za afya ya wanyama, usimamizi wa samadi ya ng‘ombe, na teknolojia nyingine za mabadiliko ya tabianchi zinazolenga kuongeza tija ya maziwa, kuimarisha ustahimilivu na kupunguza athari za mazingira zitokanazo na uzalishaji wa maziwa.
Mradi pia unaongeza uelewa wa wananchi kuhusu mnyororo wa thamani wa maziwa kwa kuonyesha jinsi mradi unavyosaidia kutoa maarifa, ujuzi, na vifaa vinavyoongeza usalama na ubora wa maziwa. Uelewa huu utahusisha mnyororo mzima wa kushughulikia maziwa.
Kuhusu C- SDTP
Mradi wa Tasnia ya Maziwa na Mabadiliko ya Tabianchi ni juhudi ya pamoja ya miaka kumi (2024-2034) kati ya Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zenye lengo la kuboresha maisha na ustahimilivu wa jamii za vijijini kupitia mabadiliko endelevu ya sekta ya maziwa.
Mradi unalenga kuwezesha wazalishaji wadogo wa maziwa kupitia uwekezaji unaojali mabadiliko ya tabianchi na unaolenga masoko na kuongeza ushiriki katika mnyororo wa thamani wa maziwa, kuongeza mapato ya kaya, kuboresha usalama wa chakula na lishe, na kukuza mifumo endelevu ya utengenezaji wa maziwa inayojali uhifadhi wa mazingira.
Mradi huu unafadhiliwa na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Mfuko wa OPEC wa Maendeleo ya Kimataifa (OFID), Mfuko wa Hali ya Hewa ya Kijani (GCF) na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).







No comments: