KAMPENI YA SAMIA LEGAL AID YATUA SHINYANGA, WANANCHI KUPATA MSAADA WA KISHERIA BURE
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita akizungumza na vyombo vya habari kuhusu kampeni ya Samia Legal Aid.***
Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga wametakiwa kuchangamkia fursa ya kupata huduma za msaada wa kisheria kupitia kampeni ya Samia Legal Aid Campaign itakayofanyika kuanzia Jumatano Mei 06, 2026 hadi Mei 20, 2026 katika halmashauri zote sita za mkoa huo bila malipo yoyote.
Akizungumza na waandishi wa habari jumanne Mei 05, 2026 Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita alisema tangu kuanzishwa kwa kampeni ya Samia Legal Aid mwaka 2023, imewasaidia wananchi wengi wa mkoa huo.
"Kwa awamu ya kwanza, wananchi 22,261 walikuwepo katika kampeni hiyo, ambapo migogoro 578 ilipokelewa, ikiwemo migogoro 317 iliyopatiwa utatuzi wa papo kwa papo na 261 iliyobaki kufanyiwa kazi" alisema Mhita.
Mhita pia alibainisha kuwa huduma hii inatolewa bure kwa siku kumi na tano kuanzia Mei 5 2026 mpaka Mei 20, 2026 katika halmashauri zote za wilaya mkoa wa Shinyanga ambazo ni Manispaa ya Shinyanga, Wilaya ya Shinyanga, Msalala, Manispaa ya Kahama, Ushetu na Kishapu.
"Katika Manispaa ya Shinyanga watakuwa eneo la Nguzo Nane katika viwanja vya zimamoto, Manispaa ya Kahama watakuwa kata ya Majengo, National Housing na kata ya Shunu eneo la ofisi ya mtendaji, Halmashauri ya Kishapu watakuwa Mhunze Mnadani na kata ya Ukenyenge, Community Centre, Msalala huduma itatolewa Segese uwanja wa shule na Isaka uwanja wa kosta na Ushetu katika kata ya Burungwa Centre na Nyamilangano Centre" alisema Mhita.
Pia amesema wanufaika wakubwa wa kampeni hii ni wananchi wa kawaida ambao hupitia changamoto mbalimbali katika utafutaji wa suluhu katika mambo ya kisheria na kwamba kampeni hiyo itawasaidia kupata njia sahihi za kufuata ili waweze kufikia malengo wanayoyakusudia ambapo Serikali imelenga kuwafikia zaidi wanawake, watoto, wazee na wenye ulemavu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Uzingatiaji wa Msaada wa Kisheria, Osborn Paissi alisema matarajio ya kampeni hiyo ni kuwafikia angalau asilimia 50 ya wananchi wenye kero za kisheria.
"Tuna matarajio ya kuwafikia asilimia 50 ya wananchi wa Shinyanga kwa huduma za utoaji elimu ya kisheria, uandaaji wa masuala ya kisheria, kutoa uwakilishi wa mahakamani katika mabaraza, usajili wa vyeti vya kuzaliwa na vifo sambamba na utoaji wa hati ya umiliki wa ardhi kwa muda mfupi" alisema Paissi.
Paissi aliongeza kuwa katika awamu ya kwanza ya mwaka 2023, asilimia 33 ya migogoro yote ilikuwa ni migogoro ya ardhi.
"Katika kipindi hiki, tumejipanga kutoa elimu ya umiliki wa ardhi na mipaka ya ardhi, jambo litakalosaidia kupunguza idadi ya migogoro ya ardhi" alisema Paissi.
Kampeni hiyo itafanyika kwa siku 15 kuanzia Mei 06 hadi Mei 20, 2026, ikihusisha timu ya wataalamu wa masuala ya kisheria.
Huduma zinazotolewa ni pamoja na ushauri wa kisheria, elimu kuhusu sheria, pamoja na uandaaji wa nyaraka za kisheria.
.jpeg)
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita.
Afisa Maendeleo Mkoa wa Shinyanga, Rehema Edson.
Mwenyekiti wa Msaada wa Kisheria Mkoa wa Shinyanga, John Shija.
Mkurugenzi Msaidizi wa uzingatiwaji wa huduma za msaada wa kisheria wa kampeni ya Samia Legal Aid, Osborn Paiss.
No comments: