WATAALAM WA MAENDELEO YA JAMII WAHIMIZWA KUELIMISHA WANANCHI ILI KUFIKIA DIRA 2050
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Maendeleo ya Vijana, Dkt. Joel Nanauka amewahimiza Maafisa Maendeleo ya Jamii kuendelea kuelimisha wananchi kushiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo ili kufikia Dira 2050 kwa ufanisi.
Waziri Nanauka ameyasema hayo jijini Mwanza Jumatano Juni 17, 2026 alipokuwa mgeni rasmi kwenye ufunguzi wa kongamano na mkutamo Mkuu wa 18 wa Chama cha Wataalam wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (CODEPATA).
Amesea maafisa hao wana nafasi kubwa katika kuunganisha wananchi, Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo ambao kwa pamoja wanasaidia kuleta mabadiliko yatakayosaidia kufikia Dira hiyo inayoanza kutumika rasmi Julai Mosi 2026.
"Mna jukumu kubwa la kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika shughuli na miradi ya maendeleo huku mkihakikisha wanatambua fursa mbalimbali zinazotolewa na Serikali" alisema Nanauka.
Naye rais wa CODEPATA, Victor Kabuje aliiomba Serikali kuongeza bajeti itakayosaidia utendaji kazi wa watumishi wa maendeleo ya jamii huku ikiendelea pia kuboresha mazingira ya kazi na muundo wa mishahara ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Kabuje alisema CODEPATA ina zaidi ya wanachama 1,820 kutoka sekta za umma na binafsi ambao wanaendelea kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Aliongeza kuwa maafisa hao waemekuwa mstari wa mbele kuhamasisha wananchi kujiunga na bima ya afya kwa wote, kupambana na matumizi ya dawa za kulevya, kuzuia matukio ya ukatili wa kijinsia hasa kwa wanawake na watoto pamoja na kuwezesha vijana, wanawake na makundi maalum kupitia fedha za mikopo ya asilimia 10 zinazotolewa na Halmashauri zote nchini.
Kabuje aliongeza kuwa amani na utulivu ni msingi wa maendeleo hivyo jamii inapaswa kuendelea kulinda amani ili kuwezesha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa vitendo.
"Utekelezaji wa Dira 2025 unahitaji wananchi kuelewa walipotoka, walipo sasa na wanapotaka kufika hivyo kama Taifa tunapaswa kushiriki kikamilifu katika kufanikisha malengo yaliyowekwa" alisema Kabuje.
Waziri wa Vijana, Dkt. Joel Nanauka
Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amir Mkalipa akitoa salamu kwenye mkutano huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum- Amon Mpanju akitoa salamu kwenye mkutano huo.
Katibu Mkuu CODEPATA, Sigilinda Mdemu akitoa salamu kwenye mkutano huo ulioambatana na uzinduzi wa Bodi ya Wadhamini ya CODEPATA.
Maafisa Maendeleo wakifuatilia mkutano huo.
Maafisa Maendeleo wakiwa kwenye mkutano huo.
Viongozi mbalimbali wakifuatilia Mkutano Mkuu wa CODEPATA ulioambatana na kaulimbiu isemayo "Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii, Chachu Kufikia Dira 2050".








No comments: