SHILINGI MILIONI 30 KUTOKA STANBIC ZAWEZESHA MASHINDANO YA 13 YA BASKETBALL YA WACHINA TANZANIA
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam, Tanzania – Jumamosi, 1 Agosti 2026: Stanbic Bank Tanzania imetoa Shilingi milioni 30 kama udhamini wa Mashindano ya 13 ya Mpira wa Kikapu ya Jamii ya Wachina nchini, katika hatua inayolenga kuimarisha mahusiano na ushirikiano kati ya benki hiyo na jamii ya Wachina.
Hafla ya ufunguzi wa mashindano hayo ilifanyika katika Viwanja vya Don Bosco, Namanga, na kufunguliwa rasmi na Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Gerson Msigwa. Katika hafla hiyo hundi ya udhamini ilikabidhiwa mbele ya Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Mheshimiwa Chen Mingjian.
Mbali na udhamini, Stanbic Bank pia imetoa timu yake kushiriki mashindanoni, jambo lililoonyesha dhamira ya benki kuwa karibu na jamii na kushiriki moja kwa moja katika shughuli zinazowaunganisha watu.
Akizungumza kabla ya ufunguzi, Mkuu wa Kitengo cha Uwekezaji (Corporate and Investment Banking) wa Stanbic Bank Tanzania, Ester Manase, alisema udhamini huo unaonyesha imani ya benki katika nguvu ya ushirikiano unaojengwa kupitia shughuli za pamoja.
"Kwa miaka mingi, mashindano haya yamekuwa moja ya majukwaa muhimu kwetu katika kuimarisha mahusiano na jamii ya Wachina nchini Tanzania kwa sababu tunaamini ushirikiano imara hujengwa kupitia uzoefu wa pamoja, si miamala ya kifedha pekee. Dhamira hiyo ndiyo msingi wa kazi yetu kupitia Standard Bank Group, ushirikiano wetu na ICBC pamoja na dawati letu maalum la huduma kwa wafanyabiashara wa Kichina," alisema.
Manase aliongeza kuwa:"Udhamini wetu wa Shilingi milioni 30 una maana kubwa zaidi ya kugharamia mashindano. Kwa kushiriki kama mdhamini na pia mshindani, tunaonyesha kuwa ushirikiano wetu ni wa dhati na wa muda mrefu. Tunaendelea kuunga mkono mipango inayokuza mshikamano wa jamii, kubadilishana tamaduni na maendeleo ya pamoja."
Kwa upande wake, Bw. Gerson Msigwa alipongeza Stanbic Bank kwa mchango wake na kusema michezo imekuwa daraja muhimu la kuimarisha urafiki kati ya Tanzania na China.
"Uhusiano kati ya China na Tanzania una historia ndefu na unaendelea kuimarika kupitia matukio kama haya ambapo michezo inatuunganisha katika roho ya urafiki na kuheshimiana. Ushirikiano wa namna hii kati ya sekta binafsi na jamii unachangia kuimarisha mahusiano kati ya wananchi wa mataifa yetu mawili," alisema.
Mashindano ya Mpira wa Kikapu ya Wachina yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kujenga mitandao ya biashara, kuimarisha mahusiano na kukuza kubadilishana uzoefu wa kitamaduni kati ya wadau kutoka Tanzania na China.
Kadri ushirikiano huo unavyoendelea kukua, Stanbic Bank itaendelea kuimarisha uhusiano wake na jamii ya Wachina nchini Tanzania pamoja na kuunga mkono majukwaa yanayochochea ushirikiano, maelewano na maendeleo ya pamoja.











No comments: