LIVE STREAM ADS

Header Ads

TRAMEPRO YATAKA VIJANA KUWA CHACHU YA MAENDELEO YA TAIFA

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Na Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania (TRAMEPRO) limewataka vijana kutumia ubunifu, sayansi na teknolojia kama nyenzo za kujenga uchumi, kuzalisha ajira na kulinda mazingira, likisisitiza kuwa wao ndiyo nguvu ya mabadiliko ya sasa na si viongozi wa kesho pekee.

Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa TRAMEPRO, Boniventura Ferdinand Mwalongo, katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yaliyofanyika Agosti 15, 2026. Amesema Tanzania ina takribani vijana milioni 20.6 wenye umri wa miaka 15 hadi 35, sawa na asilimia 34.4 ya wananchi wote kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, hivyo ni muhimu kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.

Mwalongo amesema dunia inaingia kwa kasi katika matumizi ya akili mnemba (AI), teknolojia za kidijitali, bioteknolojia na nishati jadidifu, hali inayowalazimu vijana kujikita katika maarifa, utafiti na ubunifu ili wawe wabunifu wa teknolojia badala ya kuwa watumiaji pekee wa teknolojia zinazobuniwa na wengine.

Ameeleza kuwa licha ya changamoto zinazowakabili vijana, zikiwemo ukosefu wa ajira, mitaji, ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko, taarifa potofu na athari za mabadiliko ya tabianchi, bado wana nafasi kubwa ya kubadilisha changamoto hizo kuwa fursa kupitia ujasiriamali, matumizi sahihi ya teknolojia na uwekezaji katika sekta mbalimbali za uzalishaji.

Kwa mujibu wa TRAMEPRO, ulinzi wa mazingira unapaswa kuwa sehemu ya maisha ya kila kijana kwani maendeleo endelevu hayawezi kupatikana bila kuhifadhi udongo, maji, misitu, hewa na bioanuwai. Shirika hilo limesisitiza kuwa vijana wanapaswa kuwa walinzi wa rasilimali za asili huku wakizitumia kwa busara ili kunufaisha kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha, Mwalongo amesema Tanzania ina utajiri mkubwa wa mimea tiba na maarifa ya jadi ambayo yanaweza kuwa chanzo cha ajira, utafiti na uchumi wa kijani iwapo yataendelezwa kwa kuzingatia misingi ya kisayansi, ubora na sheria. Amewahimiza vijana kujitokeza kuwekeza katika kilimo cha mimea tiba, uchakataji, uzalishaji wa bidhaa zenye thamani, teknolojia na biashara zinazohusiana na sekta hiyo.

TRAMEPRO pia imeiomba Serikali na wadau wa maendeleo kuendelea kuwekeza katika elimu, tafiti, vituo vya ubunifu, mitaji, viwanda na masoko ili kuwajengea vijana uwezo wa kujitegemea na kuzalisha ajira. Shirika hilo limehimiza familia, viongozi wa dini, wazee wa mila, mashirika ya kiraia na sekta binafsi kushiriki katika malezi na uwezeshaji wa vijana wenye maadili, maarifa na uwezo wa kushindana katika uchumi wa dunia.

Akihitimisha ujumbe wake, Mwalongo amewataka vijana kutambuliwa kwa kazi, ubunifu, uadilifu na mchango wao katika maendeleo ya taifa badala ya idadi yao, akisisitiza kuwa uwekezaji kwa vijana wa leo ndiyo msingi wa kujenga Tanzania na Afrika yenye uchumi shindani, mazingira salama na maendeleo endelevu.

No comments:

Powered by Blogger.