LIVE STREAM ADS

Header Ads

KALAMU KWA MAENDELEO: TCRA YAWAALIKA WADAU KUDHAMINI TUZO

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Na Mwandishi Wetu.

Dar es Salaam, Septemba 3, 2026: Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa wito kwa taasisi, kampuni, mashirika na wadau wa maendeleo kujitokeza kudhamini Samia Kalamu Awards 2026 ili kuunga mkono uandishi wa habari unaochochea maendeleo ya Taifa.

Wito huo umetolewa leo, Septemba 3, 2026, na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Mhandisi Peter Mwasalyanda, wakati akitangaza kufuzu kwa kazi 294 zilizoingia katika hatua ya kupigiwa kura na wananchi.

Mhandisi Mwasalyanda amesema ushiriki wa wadau kupitia udhamini ni sehemu muhimu ya juhudi za kutambua, kuenzi na kuhamasisha uandishi wa habari wenye ubora, weledi na ubunifu pamoja na maudhui yenye manufaa kwa jamii.

Amesema udhamini wa tuzo hizo utasaidia kujenga na kuimarisha mazingira yatakayowahamasisha waandishi wa habari na vyombo vya habari kuendelea kuzalisha maudhui bora, yenye taarifa sahihi na yanayozingatia maadili ya taaluma.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kuunga mkono Samia Kalamu Awards ni kushiriki katika juhudi za kukuza uandishi wa habari unaochangia maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kitaifa.

Katika msimu wa mwaka 2026, kazi 3,003 kutoka kwa waombaji 985 ziliwasilishwa kwa ajili ya kushindanishwa. Baada ya tathmini ya jopo la majaji, kazi 294 zilizopata alama za juu zimefuzu kuingia katika hatua ya kupigiwa kura na wananchi.

Naye Mwenyekiti Mwenza wa Mashindano hayo na Mkurugenzi wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben, amesema mashindano hayo yamewaleta pamoja waandishi wa habari kutoka maeneo ya vijijini na mijini, akisisitiza kuwa washiriki watashindana kwa kuzingatia ubora wa kazi zao na si umaarufu wao.

Kwa mujibu wa mmoja wa majaji wa mashindano hayo, Bi. Beatrice Bandawe, amesema kuwa miongoni mwa maeneo yaliyopatiwa kipaumbele katika kazi zilizowasilishwa ni pamoja na afya, jinsia na makundi maalum, mazingira pamoja na elimu.

Tuzo za Samia Kalamu Awards zinajumuisha makundi mbalimbali yanayowapa waandishi wa habari, maafisa habari na vyombo vya habari fursa ya kushindana kupitia kazi zilizochapishwa au kurushwa ndani ya kipindi kilichobainishwa.

Tuzo hizo zinaratibiwa na TCRA kwa kushirikiana na TAMWA na JAB, chini ya kaulimbiu ya “Kalamu kwa Maendeleo.”

No comments:

Powered by Blogger.