LIVE STREAM ADS

Header Ads

TANESCO YAMKAMATA ‘KISHOKA’ ALIYEMUUNGANISHIA MTEJA UMEME KWA MITA YA ZAMANI

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Fundi wa TANESCO Kahama akiwa juu ya nguzo ya umeme akikata nyaya za umeme zilizofungwa bila utaratibu wakati wa kumuunganishia huduma mteja.
Fundi Jamari Julius (30) akiwa ameshika mita ya umeme ya zamani inayodaiwa kufungiwa mteja kimakosa.

Na Mwandishi Wetu, Malunde1 Blog.

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Shinyanga kwa kushirikiana na wananchi, limemkamata fundi ‘kishoka’ Jamari Julius (30), mkazi wa Mhungula Manispaa ya Kahama kwa tuhuma za kumuunganishia mteja umeme kwa kutumia mita ya zamani isiyokuwa na rimoti, hatua inayodaiwa kulisababishia shirika hasara.

Aidha kukamatwa kwa fundi huyo kumefuatia taarifa iliyotolewa na mteja, Hamza Yahya (53), mkazi wa Mtaa wa Mhungula, aliyefika katika Ofisi za TANESCO Kahama kulalamikia kuunganishiwa umeme kwa kutumia mita isiyokuwa na rimoti na iliyowekwa ukutani badala ya kwenye nguzo, tofauti na utaratibu unaotumika kwa mita za kisasa.

Ofisa Usalama wa Miundombinu ya TANESCO mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Frank Njavike amesema tukio hilo lilianza baada ya kupata taarifa kutoka kwa mhasibu wa shirika katika Ofisi ya Kahama kuhusu mteja aliyefika kutoa malalamiko hayo.

Amesema taarifa hiyo ilipokelewa Septemba 23, majira ya saa 3:30 asubuhi, na baada ya kuwasiliana na mteja huyo, wataalamu wa shirika walifika katika eneo la tukio na kukagua mita iliyokuwa imefungwa na kubaini ni ya zamani na imewekwa ukutani.
“Mlalamikaji leo amewasiliana na fundi wake ‘kishoka’, akimtaka afike kwake kuchukua kiasi cha fedha kilichobaki ambacho fundi alikuwa akidai baada ya kazi. Alipofika tumemkamata kwa hatua nyingine za kisheria, kwani suala hili likiendelea linasababisha hasara kwa shirika na wateja”,ameongeza Njavike.

Njavike amesema, kukamatwa kwa fundi huyo kumefanikiwa kutokana na ushirikiano kati ya TANESCO na wananchi, ambao wamekuwa wakitoa taarifa wanapoona viashiria vya hujuma dhidi ya miundombinu ya umeme au ukiukwaji wa taratibu.

Njavike amewataka wananchi kuacha kutumia mafundi ‘vishoka’ katika kupata huduma za umeme na badala yake kufuata taratibu rasmi zilizowekwa na TANESCO kwa kupata Namba ya Malipo (Control Number) na kulipia gharama zinazotakiwa kisheria, badala ya kumpatia mtu fedha taslimu kwa ajili ya kuunganishiwa huduma.

Naye Hamza Yahaya akizungumza kuhusu tukio hilo, amesema wakati mafundi walipokuwa wakimfungia huduma ya umeme hakuwepo nyumbani, na kazi hiyo ilisimamiwa na kijana wake ambaye baadaye alimjulisha kuwa mita iliyofungwa haikuwa na rimoti na ilikuwa imewekwa ukutani.

Amesema baada ya kufika nyumbani na kushuhudia hali hiyo, aliwasiliana na fundi aliyemfungia umeme akitaka kufahamu rimoti ya mita hiyo ilikuwa wapi na angeitumiaje baada ya umeme wa mita kuisha, alipewa majibu ambayo hayakumridhisha na kuchukua hatua ya kufika ofisi za Tanesco Kahama kulalamika.

“Wataalamu wa TANESCO walipofika na kukagua, waligundua kuwa nimefungiwa mita ya zamani kimakosa. Baadaye tuliweka mtego wa kumkamata fundi wangu kwa kumuita aje kuchukua kiasi cha fedha Sh.80,000 kilichokuwa kimebaki”, amesema Yahaya.

Amesema, awali walikubaliana na fundi huyo kuhusu malipo ya Sh.600,000 kwa ajili ya kazi hiyo, na tayari alikuwa ameshalipa sehemu ya fedha hizo na kuwataka wananchi wenzake kuacha kutumia mafundi wasiokuwa na anuani na badala yake wafike ofisi za tenesco kupata huduma iliyo salama.

Hata hivyo; Baada ya kukamatwa fundi kishoka, Jamari Julius (30) amekiri kuwa alishirikiana na baadhi ya mafundi wa TANESCO Ofisi ya Kahama katika kumuunganishia mteja huyo huduma ya umeme.

Julius, amesema hakujua kuwa mita iliyofungwa kwa mteja huyo ilikuwa ya zamani na yeye ni fundi umeme wa mitaani na ndiye aliyefanya mifumo ya umeme ndani ya nyumba ya mteja huyo ambapo alilipwa Sh.450,000.

Kadhalika Julius amesema sehemu ya fedha hizo iligawanywa na mafundi wa TANESCO waliohusika katika kazi hiyo, huku yeye akisema alipokea Sh.100,000 kwa sababu alikuwa pia na fedha nyingine kutoka kwa mteja.

“Katika kazi zangu ninashirikiana na baadhi ya mafundi wa umeme wa Shirika la TANESCO. Nilipopewa fedha hii, nilimpatia fundi wa shirika anayeitwa Edward maarufu kama Mwarabu, na yeye ndiye aliyekuja na mafundi wengine wakafunga mita hii. Sasa hapa kosa langu lipo wapi, ndugu mwandishi?” amehoji Julius.

Naye Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mhungula, Nelly John amesema TANESCO inapaswa kutoa elimu kwa wananchi kuhusu taratibu sahihi za kupata huduma ya umeme ili kuwasaidia kutambua na kuepuka mafundi ‘vishoka’.

Amesema elimu hiyo inaweza kutolewa kupitia viongozi wa mitaa ambao watawafikishia wananchi taarifa kuhusu namna sahihi ya kuomba na kulipia huduma za umeme.

Nelly amesema, hata yeye aliwahi kukutana na changamoto wakati wa kutafuta huduma ya umeme, ambapo mume wake alilipa Sh.150,000 kwa ajili ya gharama ya nguzo wakati shirika lilipokuwa likisambaza nguzo katika maeneo ya mitaa huo, hata hivyo hawakuweza kupata huduma ya umeme hadi walipofuata utaratibu rasmi uliowekwa.

Ameongeza kuwa nyumba nyingi katika eneo hilo zimejengwa lakini bado hazina huduma ya umeme, hivyo baadhi ya wananchi wasioufahamu utaratibu sahihi wanaweza kuingia kwenye mikono ya watu wanaodai kuwa wanaweza kuwaunganishia huduma kinyemela.

No comments:

Powered by Blogger.