LIVE STREAM ADS

Header Ads

MIJADALA MKUTANO WA CATA IJIKITE KATIKA TEKNOLOJIA - MAKAMU WA RAIS MHE. NDEJEMBI

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Deogratius Ndejembi amesema matumizi ya mifumo ya kisasa ya teknolojia ni chachu katika ukusanyaji wa kodi hivyo yanapaswa kutiliwa mkazo ili kuongeza uwazi, kuimarisha usimamizi wa kodi na kurahisisha ulipaji kodi na kutaka mijadala ya mkutano wa 46 wa Chama cha Wasimamizi wa Kodi wa Jumuiya ya Madola (CATA) iangazie zaidi teknolojia. 

Akizungumza Makamu jijini Arusha Oktoba 06, 2026 wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa 46 wa CATA amesema teknolojia ni nyenzo muhimu katika kuboresha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuimarisha huduma kwa walipa kodi ndiyo maana mkutano huo umekuja na kauli mbiu inayogusa teknolojia.

Makamu wa Rais pia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya kodi, akibainisha kuwa biashara zinazovuka mipaka, makampuni ya kimataifa, miamala ya kidijitali pamoja na mali za kifedha zinazohifadhiwa nje ya nchi zimefanya ushirikiano kati ya mamlaka za kodi kuwa muhimu zaidi.

Awali akizungumza katika mkutano huo Rais wa CATA Mhe. Abu Tariq Jamaluddin amesema matumizi ya teknolojia ya kisasa yamekuwa yakisaidia nchi wanachama wa CATA kurahisisha utawala wa kodi kwa kuweka mazingira rahisi ya ukusanyaji wa mapato na kuwasaidia walipakodi kufuata sheria za kodi.

Kwa upande wake Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambao ndiyo waandaaji wa mkutano huo Bw. Yusuph Juma Mwenda amesema Mamlaka hiyo imepiga hatua kubwa katika matumizi ya teknolojia ambayo yameboresha zaidi huduma za usimamizi wa kodi kwa kuongeza uwazi na ufanisi.

Amesema kupitia matumizi ya teknolojia TRA imekuja na mfumo wa IDRAS unaosimamia kodi za ndani ambao unamuwezesha Mlipakodi kutoa risiti za kielektroniki kwa kutumia simu ya mkononi bila kuwa na mashine hali ambayo imeongeza uhiari katika kulipa kodi na kupunguza kuonana kwa walipakodi na maofisa wa TRA. 

Mkutano huo utadumu mpaka Oktoba 09 mwaka huu.

No comments:

Powered by Blogger.