LIVE STREAM ADS

Header Ads

MUHEZA YAVUNA MATUNDA YA KUWEKEZA KWA WAKULIMA, YASHINDA KITAIFA

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Na Mwandishi Wetu

HALMASHAURI ya Wilaya ya Muheza mkoani Tanga imewataka wawekezaji kutumia fursa zilizopo katika sekta ya kilimo kwa kuwekeza katika uzalishaji wa mazao ya kisasa na viwanda vya kuchakata bidhaa za kilimo ili kuongeza thamani na kipato cha wakulima.

Wito huo umetolewa kufuatia ushindi wa kitaifa uliotwaa na halmashauri hiyo katika Maonyesho ya Wiki ya Chakula na Lishe Duniani yaliyofanyika katika Viwanja vya Usagara, jijini Tanga, ambapo ilionesha uwezo wake katika uzalishaji wa mazao na mnyororo wa thamani kuanzia shambani hadi sokoni.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Naima Chondo, amesema ushindi huo umetokana na maandalizi mazuri na juhudi za kuwawezesha wakulima wadogo kushiriki maonyesho hayo, kujifunza teknolojia mpya za kilimo na kupata fursa ya kuonesha ubora wa mazao yao.
Amesema Muheza ina ardhi yenye rutuba inayofaa kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali, hivyo kuifanya wilaya hiyo kuwa na fursa za uwekezaji katika kilimo na biashara. Ameongeza kuwa ushiriki wa wakulima katika maonyesho hayo umewapa nafasi ya kujifunza mbinu zinazoweza kuongeza tija na thamani ya bidhaa zao.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Ayubu Sebabili, amesema wilaya hiyo imetenga maeneo kwa ajili ya kilimo cha kisasa na ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao ili kuongeza thamani ya bidhaa na kupanua fursa za ajira na biashara.

Amezitaja baadhi ya fursa zilizopo kuwa ni kilimo cha mahindi, ndizi na mazao ya viungo kama karafuu, iliki na mdalasini, ambayo yanaweza kunufaisha wakulima na wafanyabiashara kupitia masoko ya ndani na nje ya nchi.
Sebabili amesema wilaya hiyo inapanga kufanya kongamano la wadau wa kilimo litakalowakutanisha wakulima, wafanyabiashara, taasisi za fedha na wawekezaji ili kuweka mikakati ya pamoja kuelekea msimu ujao wa kilimo.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dkt. Batilda Buriani, amesema mkoa huo una fursa za kiuchumi zinazohusishwa na upanuzi wa Bandari ya Tanga, Bomba la Mafuta na uwekezaji katika kilimo na viwanda. Amewahimiza wawekezaji kutumia fursa hizo kuongeza uzalishaji wa chakula na kukuza uchumi.

Dkt. Buriani ametoa shukrani kwa Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Shirika la Chakula Duniani (WFP) na wadau wengine walioshiriki maonyesho hayo yenye kaulimbiu isemayo “Ubunifu wa Leo, Lishe Bora ya Kesho, Kuelekea Dira 2050.”

No comments:

Powered by Blogger.