DCEA YATWAA TUZO YA NBAA KWA UBORA WA TAARIFA ZA HESABU
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeibuka mshindi wa kwanza katika kundi la Taasisi za Serikali zinazojitegemea na kutunukiwa Tuzo ya Umahiri wa Uandaaji Bora wa Taarifa za Hesabu kwa mwaka 2024/2025.
Tuzo hiyo inayotolewa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), inatambua ubora na uzingatiaji wa Viwango vya Kimataifa vya Uhasibu katika Sekta ya Umma (IPSAS) katika uandaaji wa taarifa za hesabu.
Akizungumzia ushindi huo, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema tuzo hiyo ni utambuzi wa ubora, weledi na uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za umma, na inathibitisha dhamira ya Mamlaka ya kuhakikisha rasilimali inazopatiwa zinasimamiwa kwa uadilifu, uwazi na kuleta tija katika utekelezaji wa majukumu yake ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya.
Amewapongeza na kuwashukuru watumishi wote wa DCEA, hususan Kitengo cha Fedha na Uhasibu pamoja na Kitengo cha Ukaguzi wa Ndani, kwa kujituma na kushirikiana kufanikisha ushindi huo.
DCEA itaendelea kuimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha, uwazi na uwajibikaji, kwa kuhakikisha kila rasilimali ya umma inatumika kwa ufanisi na kuleta thamani kwa wananchi.












No comments: