NAIBU WAZIRI MKAMA NA UJUMBE WA TANZANIA WAENDELEZA MIJADALA SIKU YA PILI MKUTANO WA PAPU
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Switbert Zacharia Mkama (Mb), ameongoza ujumbe wa Tanzania katika siku ya pili ya Mkutano wa 11 wa Mawaziri wa Umoja wa Posta Afrika (11th PAPU Plenipotentiary Conference) uliofanyika Machi 26, 2026, jijini Kampala.
Katika mkutano huo, Mhe. Dkt. Mkama ameambatana na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Mohamed Sijamini Mohamed, pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Bw. Nicholas Merinyo Mkapa, wakishiriki kama chombo kikuu cha maamuzi kwa ajili ya mustakabali wa huduma za posta barani Afrika.
Viongozi hao wamefuatilia kwa kina mijadala ya mada mbalimbali zilizolenga kufanya mageuzi makubwa ya sekta ya posta ili kuendana na kasi ya maendeleo ya kidijitali na mifumo ya kisasa ya usafirishaji (logistics).
Lengo kuu la mijadala hiyo ya siku ya pili lilikuwa ni kuweka mikakati thabiti ya kuimarisha ushirikiano miongoni mwa nchi wanachama, huku Tanzania ikisisitiza umuhimu wa kuboresha huduma za mipakani ili kuchochea biashara ya mtandaoni (e-commerce) na kurahisisha mawasiliano kwa wananchi wa hali ya chini barani kote.
Ushiriki wa viongozi hawa waandamizi kutoka pande zote mbili za Muungano unadhihirisha utayari wa Tanzania katika kusimamia maazimio yatakayopitishwa kuelekea uchaguzi wa uongozi mpya wa PAPU.
Mkutano huu unatarajiwa kuhitimishwa kwa kuweka misingi imara ya kisheria na kisera itakayobadilisha sekta ya posta kuwa mhimili wa kiuchumi, huku ukiondoa vikwazo vya kizamani na kutengeneza fursa mpya za ajira kupitia mifumo ya usambazaji wa bidhaa na huduma za kiteknolojia.
Na Dotto Manumbu, Kampala- Uganda




No comments: