LIVE STREAM ADS

Header Ads

NAIBU WAZIRI MKAMA ASHIRIKI MKUTANO WA 11 WA PAPU KUIMARISHA SEKTA YA POSTA AFRIKA

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ukerewe, Mhe. Switbert Zacharia Mkama, ameshiriki katika Mkutano wa 11 wa Mawaziri wenye Mamlaka Kamili wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU) uliofanyika jijini Kampala, nchini Uganda kuanzia tarehe 25 hadi 27 Machi, 2026.

Mhe. Mkama amewakilisha Tanzania katika chombo hicho cha juu kabisa cha maamuzi, ambacho kimekutanisha Mawaziri wanaohusika na huduma za posta kutoka nchi wanachama barani kote ili kuweka mwelekeo mpya wa sekta hiyo.

​Lengo kuu la ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo lilikuwa ni kushiriki kwenye mijadala ya kimkakati inayolenga kuboresha ushirikiano miongoni mwa waendeshaji wa huduma za posta barani Afrika.

Aidha, Mhe. Mkama amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kufanya kazi kwa pamoja ili kuhakikisha huduma za posta zinavuka mipaka kwa ufanisi zaidi, jambo litakalochochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali na biashara ya mtandaoni (e-commerce) ndani ya bara hili.

​Katika mkutano huo, viongozi hao wamepitia hatua zilizopigwa katika utekelezaji wa sera na mipango mkakati ya PAPU, huku wakijadili mbinu za kisasa za kukabiliana na changamoto za sasa.

Aidha, wajumbe wamefanikiwa kupitisha maazimio na mwelekeo wa sera yatakayotoa dira ya mustakabali wa Sekta ya Posta barani Afrika kwa miaka ijayo, yakilenga kuifanya sekta hiyo kuwa yenye ushindani zaidi duniani.

​Moja ya hatua muhimu iliyofikiwa ni mjadala wa kina kuhusu mikakati ya kuibadilisha sekta ya posta kutoka mfumo wa zamani na kuwa mfumo wa kisasa wa kidijitali na usafirishaji (logistics).

Mhe. Mkama amebainisha kuwa mabadiliko haya ni lazima ili kutoa huduma zinazoendana na kasi ya teknolojia, ambapo posta haitakuwa tu sehemu ya kutuma barua, bali kitovu cha usambazaji wa bidhaa na huduma mbalimbali za kiteknolojia kwa wananchi.

​Vilevile, mkutano huo umekamilisha mchakato wa kidemokrasia kwa kuchagua uongozi mpya wa PAPU, ikiwa ni pamoja na nafasi za Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu.

Uchaguzi huu unatarajiwa kuleta damu mpya na ari ya utendaji itakayosimamia utekelezaji wa mipango yote iliyopitishwa, huku Tanzania ikiendelea kuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono juhudi za kuunganisha Afrika kupitia mawasiliano ya posta.
Na Dotto Manumbu, Kampala- Uganda

No comments:

Powered by Blogger.