LIVE STREAM ADS

Header Ads

MWANZA JIJI WATAKIWA KUTETEA UBINGWA WA MASHINDANO YA UMISSETA 2026

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Katibu Tawala Wilaya ya Nyamagana, Thomas Salala akifungua mashindano ya UMISSETA 2026 jijini Mwanza.
***

Mashindano ya michezo kwa shule za Sekondari (UMISSETA) ngazi ya Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, yameanza rasmi katika viwanja vya Shule ya Sekondari Nsumba.

Mashindano hayo yamefunguliwa Jumatatu Aprili 27, 2026 na Katibu Tawala Wilaya ya Nyamagana, Thomas Salala aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi.

Akizungumza kwenye ufunguzi huo, Salala aliwahimiza wasimamizi kuhakikisha wanatenda haki kwa kuchagua washiriki bora watakaounda timu zitakazoleta ushindani katika mashindano ya kimkoa na kitaifa ili Nyamagana na Mkoa wa Mwanza kuendelea kutetea ubingwa wao.

Pia alisisitiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kuhakikisha kupitia wasaidizi wake kuhakikisha vipaji vitakavyoibuliwa kwenye mashindano vinaendelezwa kwani michezo inatoa fursa mbalimbali ikiwemo ajira.

Naye Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Mwl. Deus Toga akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Kiomoni Kibamba aliwataka washiriki kuhakikisha wanadumisha nidhamu kwani ndio msingi wa kufanya vizuri.

Kwa upande wake Afisa Michezo Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Mohamed Bitegeko alisema mwaka huu Halmashauri hiyo imejiandaa vyema katika mashindano hayo ili kutoa wawakilishi kuendelea kutetea nafasi yake ya kwanza katika mashindano ya kimkoa na wawakilishi watakaotetea pia nafasi ya kwanza kitaifa katika mashindano yanayotarajia kuanza Juni Mosi 2026.

Ili kuboresha zaidi mashindano hayo, Mratibu wa UMISSETA Wilaya ya Nyamagana, Mtesigwa Bulenga aliomba Serikali kuendelea kuboresha viwanja vya michezo, kutoa mafunzo kwa waalimu wa michezo, kushirikisha wadau mbalimbali wa michezo na kuongeza bajeti ili kukidhi mahitaji ya mashindano.

Michuano hoyo inahusisha michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa mikono, mpira wa kikapu, mpira wa wavu, mpira wa meza, mpira wa kengele kwa wenye uono hafifu, riadha, sanaa za maonesho, usafi na nidhamu.

Kaulimbiu ya mashindano hayo mwaka huu inasema "michezo na sanaa shuleni- ni daraja la ajira na afya. Tushindaji wa kimataifa kujenga heshima na kuinua uchumi wa Taifa letu imara"
Na George Binagi- GB Pazzo, BMG
Afisa Elimu Sekondari Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Mwl. Deus Toga akizungumza kwenye ufunguzi huo.
Afisa Michezo Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Mohamed Bitegeko akizungumza kwenye ufunguzi wa UMISSETA 2026.
Mratibu wa UMISSETA Wilaya ya Nyamagana, Mtesigwa Bulenga akisoma risala ya mashindano hayo.
Washiriki wa mashindano ya UMISSETA 2026 jijini Mwanza.
Tazama picha mbalimbali za ufunguzi wa UMISSETA 2026 jijini Mwanza.
TAZAMA VIDEO HAPA CHINI

No comments:

Powered by Blogger.