LIVE STREAM ADS

Header Ads

MWENGE WA UHURU WAKAGUA TANKI LA BUHONGWA, WANANCHI ZAIDI YA 80,000 KUNUFAIKA

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Ndugu Wazo Mwang’onda, ametembelea na kukagua utekelezaji wa Tanki la Kuhifadhia Maji la Buhongwa, jijini Mwanza, na kueleza kuridhishwa na hatua ya utekelezaji wa mradi huo unaolenga kuboresha huduma ya maji kwa wananchi zaidi ya 80,000 wa Buhongwa na maeneo ya jirani.

Tanki hilo lenye ujazo wa lita milioni 10 na thamani ya takribani Shilingi bilioni 3.3, limefikia asilimia 85 ya utekelezaji na litasaidia kuhifadhi na kusambaza maji kutoka Chanzo cha Maji cha Butimba kwa wananchi wa Buhongwa, Sahwa, Kanindo, Kagera, Igwambiti, Nyashishi na Nyahingi.

Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Ndugu Mwang’onda ameipongeza MWAUWASA kwa kusimamia utekelezaji wa mradi huo na kutumia fedha za Serikali kwa lengo lililokusudiwa, huku akiielekeza Mamlaka kuendelea kumsimamia Mkandarasi ili mradi ukamilike kwa wakati na kwa kiwango kinachokubalika.
Aidha amewataka wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya maji kwa kuhakikisha hailindwi tu wakati wa utekelezaji, bali inaendelea kutunzwa ili iweze kutoa huduma kwa muda mrefu.

"Mradi wa Tanki la Buhongwa ni sehemu ya Mradi wa Ujenzi wa Matenki Matano, Ulazaji wa Mabomba Makuu ya Kusafirisha Maji na Vituo Viwili vya Kusukuma Maji, unaotekelezwa kupitia Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira ya Ziwa Victoria kwa gharama ya Shilingi bilioni 46.2 bila VAT. Mradi nahusisha matenki yenye jumla ya ujazo wa lita milioni 31 pamoja na mabomba makuu yenye urefu wa kilomita 40.5." Ameeleza Mhandisi Nuhu Said Msimamizi wa miradi MWAUWASA

Utakapokamilika, mradi unatarajiwa kuboresha huduma ya maji kwa takribani wananchi 450,000 katika Jiji la Mwanza na maeneo ya pembezoni.

MWAUWASA inaendelea kuhakikisha uwekezaji huu unazalisha matokeo yanayolenga kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi, sambamba na kutimiza azma ya Serikali ya kuimarisha huduma za msingi kwa maendeleo ya wananchi.
TAZAMA VIDEO HAPA CHINI

No comments:

Powered by Blogger.