LIVE STREAM ADS

Header Ads

RAIS SAMIA AWAPUNGUZIA ADHABU WAFUNGWA 1,369, WENGI WAACHIWA HURU

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mwandishi Wetu, DODOMA, Aprili 26, 2026

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametumia mamlaka yake ya kikatiba kutoa msamaha wa kupunguza adhabu kwa wafungwa 1,369 nchini, ambapo wafungwa 436 wameachiwa huru mara moja huku wengine 933 wakipunguziwa vifungo vyao.

Uamuzi huo umetangazwa leo jijini Dodoma na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobass Katambi, ambaye amesema hatua hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Katambi amesema msamaha huo umetolewa kwa mujibu wa Ibara ya 45(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayompa Rais mamlaka ya kutoa msamaha kwa wafungwa wanaostahili.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, walionufaika na msamaha huo ni pamoja na wafungwa waliotumikia sehemu ya vifungo vyao kwa mujibu wa sheria, wagonjwa mahututi waliothibitishwa kitaalamu, wazee wenye umri wa miaka 70 na zaidi, pamoja na wanawake wajawazito au wenye watoto wachanga waliopo magerezani.

Aidha, wafungwa waliokuwa wakitumikia adhabu ndefu, wakiwemo waliokaa gerezani kwa miaka 25 na zaidi pamoja na waliokuwa chini ya kizuizi kwa muda mrefu, nao wamejumuishwa baada ya kufanyiwa tathmini maalum.

Hata hivyo, Serikali imeeleza kuwa msamaha huo haukuwahusu wafungwa waliopatikana na hatia ya makosa mazito ikiwemo ugaidi, uharamia, ubakaji, biashara ya binadamu, rushwa, uhujumu uchumi, pamoja na wanaotumikia kifungo cha maisha.

Pia wafungwa waliowahi kunufaika na msamaha wa Rais hapo awali hawakujumuishwa katika orodha ya walionufaika safari hii.

Serikali imesema hatua hiyo inalenga kutoa nafasi ya pili kwa wafungwa waliorekebika ili warejee katika jamii na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya taifa.

“Ni matarajio ya Serikali kuwa wale walioachiwa huru watarejea katika jamii wakiwa na nidhamu, wakijihusisha na shughuli halali za kiuchumi na kuepuka kurejea kwenye vitendo vya uhalifu,” ilieleza taarifa hiyo.

Hatua hiyo imepokelewa na wananchi kama ishara ya huruma na dhamira ya Serikali ya kuendelea kuimarisha haki, utu na mageuzi ya mfumo wa marekebisho ya tabia nchini.

Wachambuzi wa masuala ya kijamii wanasema msamaha huo pia utasaidia kupunguza msongamano magerezani na kuongeza ufanisi wa huduma za marekebisho.

Maadhimisho ya miaka 62 ya Muungano yanaendelea kuambatana na hatua mbalimbali za kijamii na kiuchumi zinazolenga kuimarisha mshikamano wa kitaifa na ustawi wa wananchi

No comments:

Powered by Blogger.