LIVE STREAM ADS

Header Ads

SERIKALI YAKUTANA NA WADAU KUJADILI MIKAKATI YA KUIMARISHA MASLAHI YA WATU WENYE ULEMAVU TANZANIA

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com

Na Mwandishi Wetu-Dar es Salaam.

Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) imekutana na Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu, viongozi wa vyama vya watu wenye ulemavu pamoja na wawakilishi wa watu wenye ulemavu kutoka Mikoa mbalimbali ya Tanzania bara kwa lengo la kujadili masuala yanayohusu ustawi wa watu wenye ulemavu nchini, Tarehe 17 Aprili 2026, jijini Dar es Salaam.

Kikao hicho kimelenga kujadili na kuimarisha uelewa kuhusu Mwongozo wa Uratibu wa Vyama vya Watu Wenye Ulemavu,kujadili rasimu ya Mwongozo wa Kitaifa wa Viwango vya Ufikivu, pamoja na kuongeza uelewa juu ya utekelezaji wa fursa ya asilimia 30 ya manunuzi ya umma kwa makundi maalum.

Akifungua kikao hicho, kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Watu Wenye Ulemavu, Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (SBUU), Bw. Bruno Mwakibibi, amesema kuwa Serikali inaendelea kujenga mazingira wezeshi na rafiki kwa kushirikiana na vyama vya watu wenye ulemavu ili kuongeza ustawi wa kundi hilo.

Aidha,amesisitiza umuhimu wa viongozi hao kuendeleza umoja, mshikamano na upendo ili kuhakikisha malengo ya kuwainua watu wenye ulemavu yanafikiwa sambamba na hilo amebainisha kuwa lengo kuu la hivyo ni kuwaunganisha wanachama, jamii na Serikali kwa manufaa ya pamoja.

Aliendelea kusema kuwa, mwongozo huo, pamoja na sera, sheria na kanuni zilizopo, unalenga kuongeza ushiriki na ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, ajira, siasa na afya, huku ukihakikisha hakuna kundi linaloachwa nyuma.

Akiwasilisha rasimu ya Mwongozo wa Viwango vya Ufikivu, Afisa Sheria kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Jacob Mwinula, amesema kuwa ufikivu unahusisha kuboresha mazingira, huduma na taarifa ili ziwe rafiki na kuwawezesha watu wenye ulemavu kuishi kwa kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika jamii.

Aliongeza kuwa, mwongozo huo wa kitaifa wa Viwango vya ufikivu unalenga kuweka viwango mahsusi vya ufikivu katika sekta mbalimbali, kuchochea ushiriki jumuishi na wenye tija, pamoja na kuhakikisha mazingira yanakuwa fursa kwa watu wenye ulemavu badala ya vikwazo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu, Bi. Tungi Mwanjala, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa elimu kuhusu fursa zilizopo kwa watu wenye ulemavu na kupokea maoni yao kuhusu changamoto wanazokutana nazo.

Amewahimiza washiriki kutumia kikamilifu fursa ya asilimia 30 ya manunuzi ya umma ili kuboresha hali zao za maisha na kuongeza ushiriki wao katika shughuli za kiuchumi.

No comments:

Powered by Blogger.