SERIKALI YAONGEZA NGUVU KWA WACHIMBAJI WADOGO, YASISITIZA USALAMA MIGODINI
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
#Wakaguzi wakuu wa migodi watakiwa kupewa fursa zaidi kuimarisha usalama na utunzaji wa mazingira
**
Serikali imeendelea kusisitiza umuhimu wa kuwawezesha Wakaguzi Wakuu wa Migodi pamoja na wachimbaji wadogo nchini ili kuimarisha usalama kazini, kulinda mazingira na kuongeza mchango wa sekta ya madini katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Wito huo umetolewa leo Aprili 23, 2026 wilayani Kahama, mkoani Shinyanga na Mkurugenzi wa Huduma za Leseni wa Tume ya Madini, Mhandisi Aziza Swedi, alipokuwa akifungua mafunzo kwa mameneja na Wakaguzi Wakuu wa Migodi ya uchimbaji mdogo kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Ramadhani Lwamo.
Mafunzo hayo yanawakutanisha washiriki kutoka mikoa ya kimadini ya Kahama, Mbogwe na Shinyanga yakilenga kuimarisha uelewa wa kitaalam, usimamizi bora wa migodi, uzingatiaji wa sheria na kanuni pamoja na kukuza uchimbaji salama na endelevu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Mhandisi Swedi amesema Wakaguzi Wakuu wa Migodi wanapaswa kupewa ushirikiano na mazingira wezeshi ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu, hatua itakayosaidia kuzuia ajali migodini, kulinda afya za wachimbaji na kuhifadhi mazingira yanayozunguka maeneo ya uchimbaji.
Amesema mafanikio ya jitihada za Serikali katika kuwawezesha wachimbaji wadogo yanategemea ushirikiano wa wadau wote, hususan mameneja na wakaguzi wa migodi ambao ni nguzo muhimu katika kusimamia uzingatiaji wa sheria, kanuni na viwango vya usalama.
“Serikali inalenga kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinaendelea kuchangia maendeleo ya Taifa huku zikifanyika kwa njia salama zisizoathiri mazingira, afya za wachimbaji na ustawi wa jamii,” amesema.
Aidha, amesema kupitia usimamizi madhubuti, nchi inaweza kufikia azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuongeza mchango wa sekta ya madini katika Pato la Taifa kutoka asilimia 10 ya sasa hadi asilimia 12.5 ifikapo mwaka 2030.
Ameeleza kuwa wachimbaji wadogo tayari wanachangia takribani asilimia 40 ya mapato yatokanayo na shughuli za madini, hali inayoonesha umuhimu wao katika uchumi wa Taifa, huku akiwataka wamiliki wa migodi kuhakikisha taarifa za uzalishaji na kumbukumbu muhimu zinatunzwa ipasavyo ili Serikali ipate mapato stahiki kwa wakati.
Mhandisi Swedi pia ameonya kuhusu athari za uchimbaji usiozingatia taratibu, akitaja matumizi holela ya kemikali hatarishi kama zebaki na sayanaidi pamoja na vumbi la silica kuwa chanzo cha magonjwa hatari ikiwemo silicosis, kifua kikuu na saratani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira kutoka Tume ya Madini, Mhandisi Hamisi Kamando, amesema Wakaguzi Wakuu wa Migodi wanapaswa kuwasilisha taarifa za ukaguzi mara kwa mara ili kuiwezesha Serikali kubaini mapema vihatarishi vinavyoweza kusababisha ajali na kuchukua hatua za kinga kwa wakati.
Amesema bado kuna changamoto katika baadhi ya maeneo ya migodi ikiwemo ukiukwaji wa sheria, ukosefu wa kumbukumbu sahihi za uzalishaji, ukwepaji wa kodi na utoroshaji wa madini, hivyo mafunzo hayo yanalenga kuwajengea washiriki uwezo wa kuwa mabalozi wa uzingatiaji wa sheria na taratibu za sekta hiyo.
“Tunataka kuona wachimbaji wanaingia migodini salama na kurejea majumbani mwao salama kila siku. Uhai wa binadamu una thamani kubwa kuliko madini,” amesema Mhandisi Kamando.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini Mkoa wa Shinyanga (SHIREMA), Hamza Tandiko, amesisitiza umuhimu wa weledi kwa wachimbaji na utoaji wa taarifa sahihi za shughuli za uchimbaji, huku akipongeza mchango wa wakaguzi katika kupunguza ajali na madhara migodini.















No comments: