LIVE STREAM ADS

Header Ads

MAONESHO YA SIKU YA ZIWA VICTORIA YAANZA JIJINI MWANZA

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda (kushoto) akikagua banda la Shirika la EMEDO kwenye maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Ziwa Victoria yanayofanyika uwanja wa Nyamhongoji kuanzia Mei 18- 21, 2026.
***

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amefungua rasmi maonesho ya Siku ya Ziwa Victoria yanayofanyika kwa mara ya kwanza mwaka huu katika uwanja wa Nyamhongolo jijini Mwanza.

Mtanda amefungua maonesho hayo Jumatatu Mei 18, 2026 na kutumia fursa hiyo kusisitiza kuwa maisha ya wananchi yanategemea uwepo wa Ziwa Victoria katika shughuli mbalimbali ikiwemo za kiuchumi na kijamii hivyo ni muhimu rasilimahi hiyo kulindwa.

"Mustakabali wa maisha ya binadamu unategemea kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa maji huku ziwa Victoria likiwa mhimili muhimu wa uchumi na maendeleo ya jamii za ukanda wa Afrika Mashariki" amesisitiza Mtanda.

Mtanda amesema Bonde la Ziwa Victoria lina mchango mkubwa katika shughuli za kiuchumi na kijamii hivyo wananchi wanapaswa kushirikiana katika kulihifadhi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha Mtanda amesema Serikali kupitia Wizara ya Maji na Ofisi ya Makamu wa Rais- Mazingira imesaidia uhifadhi wa Ziwa Victoria kwa kutoa fedha za kudhibiti magugu maji na kwamba jitihada za kufanya utafiti na ununuzi wa mitambo ya kusafisha ziwa zinaendelea.

Mtanda ameongeza kuwa uhifadhi wa Ziwa Victoria utasaidia kuongeza upatikanaji wa maji kwa wananchi na pia kukuza shughuli za kiuchumi ikiwemo uzalishaji wa samaki kwa njia ya vizimba.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Rose Ambrose amesema hakuna nchi inayoweza kuhifadhi Ziwa Victoria peke yake hivyo ushirikiano wa kikanda ni muhimu ambapo maadhimisho hayo ni sehemu ya kuhimiza ushiriki wa pamoja wa utunzaji wa ziwa hilo.

Kilele cha Siku ya Ziwa Victoria itaadhimishwa Mei 21, 2026 kwa mara ya kwanza ikiwa ni azimio la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), kupitia kikao cha Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC) kilichoketi mwaka uliopita 2025 nchini Kenya, lengo likiwa ni kuhamasisha uhifadhi wa ziwa hilo kwa matumizi endelevu kiuchumi na kijamii.
Na George Binagi, Mwanza
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Rose Ambrose.
Katibu Mtendaji Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria, Masinde Bwire.
Viongozi mbalimbali meza kuu wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda.
Wananchi.

No comments:

Powered by Blogger.