MCHENGERWA ASISITIZA BIMA YA AFYA KWA WOTE BAJETI YA MWAKA 2026/27
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa amesisitiza kwamba bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27 inapaswa kutoa mwelekeo wa Taifa katika utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote.
Mchengerwa amesema hayo Jumapili Mei 03, 2026 wakati akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Wizara ya Afya kilichofanyika ukumbi wa Rock City Mall jijini Mwanza.
"Lazima tujiandae kikamilifu kwa utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote. Hili si suala la kadi pekee bali lazima kuwe na utayari wa miundombinu, mifumo, dawa na rasilimali watu imara" alisema Mchengerwa.
Mchengerwa alisisitiza kwamba lazima mifumo ya TEHAMA iwe imara, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba uimarishwe huku akiweka mkazo kwa buzalishaji wa ndani kupewa kipaumbele na Wizara ya Afya.
"Lazima mifumo ya manunuzi itoe kipaumbele kwa wazalishaji wa ndani. Katibu Mkuu nakuagiza usimamie hilo, ununuzi kupitia MSD na mifumo yetu ya manunuzi lazima izingatie hilo lakini kwa kuzingatia ubora" ameongeza.
Mchengerwa aliongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026, Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanikiwa kupiga hatua ikiwemo kuongeza upatikanaji wa dawa muhimu kufikia wastani wa asilimia 73 kwa mwezi Februari, 2026.
"Pia tumeendelea kupunguza vifo vya akina mama wajawazito kupitia uwekezaji katika vituo vya afya, hospitali za wilaya, vifaa tiba na rasilimali watu. Haya ni mafanikio ya pamoja chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan" alisema Mchengerwa.
Pia alitoa wito kwa kila mtumishi, kuanzia makao makuu hadi hospitali za rufaa, kutoka idara hadi kituo cha afya, kuhakikisha wanatoa huduma kwa weledi na huruma kwa wananchi.
"Hatutavumilia ucheleweshaji wa huduma usio na sababu. Hatutavumilia upendeleo unaodhalilisha haki za mwananchi" alisisitiza Mchengerwa huku akiagiza Katibu Mkuu kufanyia kazi malalamiko ya wagonjwa kukaa muda mrefu bila kupata huduma katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt Seif Shekalaghe alisema kikao hicho kimelenga kujadili na kupitisha mwelekeo wa bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27 yenye lengo la kuboresha huduma za afya kwa wananchi pamoja na ustawi wa watumishi.
Naye Katibu wa Baraza hilo, Vivian Joseph ambaye ni Afisa Tawala Mkuu Wizara ya Afya alisema kupitia kikao hicho kitasaidia upatikanaji wa bajeti ambayo ni shirikishi kutekelezwa na watumishi wa wizara hiyo baada ya kupitishwa na bunge.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha baraza kuu la wafanyakazi wa wizara hiyo kilichofanyika jijini Mwanza.
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa akizungumza kwenye ufunguzi wa kikao cha baraza kuu la wafanyakazi wa wizara hiyo kilichofanyika jijini Mwanza.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe akizungumza kwenye kikao cha baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo kilicholenga kujadili na kupitisha bajeti ya mwaka 2026/27.
Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe akizungumza kwenye kikao cha baraza la wafanyakazi Wizara ya Afya kilichoketi jijini Mwanza.
Wafanyakazi wa Wizara ya Afya wakifuatilia kikao cha baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo.
Wafanyakazi wa Wizara ya Afya wakifuatilia kikao cha baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo.
Wafanyakazi wa Wizara ya Afya wakifuatilia kikao cha baraza la wafanyakazi wa wizara hiyo.








No comments: