LIVE STREAM ADS

Header Ads

SERIKALI KUIMARISHA USULUHISHI WA MIGOGORO YA NDOA KABLA YA TALAKA

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imeanzisha programu maalum ya kuwajengea uwezo wajumbe wa bodi za usuluhishi wa ndoa nchini, hatua inayolenga kuimarisha utatuzi wa migogoro ya ndoa kwa njia ya maelewano kabla ya mashauri hayo kufikishwa mahakamani kwa ajili ya talaka.

Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Zainab Katimba amesema hayo bungeni leo Mei 7, 2026 alipokuwa akijibu swali kuhusu hatua zinazochukuliwa na serikali katika kuimarisha taasisi ya ndoa na kushughulikia migogoro ya kifamilia.

Amesema utekelezaji wa programu hiyo ulianza rasmi Aprili 8, 2026 katika Mkoa wa Kagera, huku lengo kuu likiwa kuhakikisha wajumbe wa bodi za usuluhishi wanapata mafunzo na uwezo wa kusaidia wanandoa kupata suluhu stahiki kabla ya kuwasilisha mashauri yao mahakamani.

“Msingi wa programu hii ni kuhakikisha migogoro ya ndoa inatatuliwa kwa njia ya usuluhishi na maridhiano ili kulinda taasisi ya ndoa,” amesema Katimba.

Akifafanua zaidi, Katimba amesema kifungu cha tisa cha Sheria ya ndoa Sura ya 29 kinatafsiri ndoa kuwa ni muunganiko wa mwanamke na mwanaume kwa lengo la kuishi pamoja maisha yao yote, jambo ambalo limeifanya sheria kuweka utaratibu wa mashauri ya ndoa kuanza kusikilizwa katika bodi za usuluhishi kabla ya kufikishwa mahakamani kwa ajili ya maombi ya talaka.

Aliongeza utaratibu huo umewekwa mahsusi ili kutoa nafasi kwa wanandoa kusuluhishwa na kurejesha maelewano badala ya kuharakisha kuvunjika kwa ndoa.

Katika hatua nyingine, Mhe. Katimba amesema Mahakama ya Tanzania imeweka mwongozo wa muda wa usikilizaji wa mashauri mbalimbali ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wakati.

No comments:

Powered by Blogger.