MWANZA: HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA ROYAL YAZINDULIWA
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Hospitali mpya ya Rufaa ya Kanda Royal iliyopo eneo la Ghana jijini Mwanza, imefunguliwa rasmi jijini Mwanza, ikiwa na matarajio ya kutoa huduma bora za afya kwa wananchi, hususan wakazi wa Kanda ya Ziwa.
Akizungumza Mei 10, 2026 wakati wa hafla ya uzinduzi wa hospitali hiyo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG), Dkt. Barnabas Mtokambali alisema Royal Hospital imeonesha uthubutu, imani na nidhamu ya kiutendaji katika safari yake ya kuwa miongoni mwa hospitali bora za kikanda hapa nchini.
Askofu Dkt. Mtokambali alisema maono ya taasisi hiyo hayakuishia kwenye karatasi, bali yamegeuka kuwa mageuzi halisi katika utoaji wa huduma bora za matibabu kwa wananchi.
Aidha alisisitiza umuhimu wa maadili, taaluma na utumishi wa kujituma katika sekta ya afya, akibainisha kuwa afya ya binadamu ni jambo nyeti linalohitaji uwajibikaji mkubwa.
Pia aliwahimiza wananchi, hususani wakazi wa Kanda ya Ziwa kutumia huduma za hospitali hiyo kwa kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara ili kusaidia kugundua hali zao za kiafya mapema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jospitali ya Royal, Dkt. Glory Simon alisema hospitali hiyo ilisajiliwa rasmi Machi 16, 2026 na kupandishwa hadhi kutoka hospitali ya Wilaya hadi kuwa hospitali ya rufaa ya kanda baada ya kupitia ukaguzi mbalimbali uliofanyika mwaka 2026.
Alieleza kuwa ujenzi wa awamu ya kwanza ulianza mwaka 2022, huku hatua za ukamilishaji wa majengo pamoja na ununuzi wa vifaa tiba zikiendelea hadi mwaka 2024.
"Kwa sasa tuna uwezo wa kuhudumia wateja 200 kwa siku, tukiwa na madaktari70, tofauti na hapo awali ambapo tulikuwa tukihudumia wateja 80 tukiwa na madaktari 30" alisema Dkt. Simon.
Dkt. Simon alibainisha kuwa ospitali hiyo imeongeza huduma na miundombinu kwa kuongeza idadi ya vitanda kutoka 10 hadi 80, vyumba vya upasuaji kutoka kimoja hadi vitano, maduka ya dawa kutoka moja hadi matatu huku idadi ya wafanyakazi ikiongezeka kutoka 70 hadi matarajio ya kufikia 300.
Nao baadhi ya wananchi na wadau mbalimbali waliojitokeza kushuhudia uzinduzi huo akiwemo Tuse mwaikasu, Martina Kabisama na Moses Tahema walipongeza ujio wa hospitali hiyo wakisema itasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali zenye hadi ya rufaa Kanda ya Ziwa.
Hospital ya Rufaa ya Kanda Royal iliyopo Mtaa wa Ghana jijini Mwanza, inatoa huduma za kawaida, kibingwa na matibabu muhimu kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza na maeneo ya Kanda ya Ziwa.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Royal jijini Mwanza, Dkt. Glory Simon.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Royal jijini Mwanza., Dkt. Lusako Mwaikasu
Afisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Royal jijini Mwanza., Dkt. Lusako Mwaikasu






No comments: