EMEDO, WADAU WAADHIMISHA SIKU YA KUZUIA KUZAMA MAJI DUNIANI 2026
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEDO) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, limeadhimisha Siku ya Kuzuia Kuzama Maji Duniani mwaka huu 2026.
Kwa mara ya kwanza duniani maadhimisho hayo yalifanyika Julai 25, 2021 kufuatia tamko la Umoja wa Mataifa (UN) la Aprili 2021 hivyo mwaka huu ni maadhimisho ya sita.
Maadhimisho hayo yamefanyika kwa mara ya kwanza jijini Mwanza, yakiwaleta pamoja viongozi na wadau mbalimbali kujadili na kuweka mikakati ya pamoja itakayosaidia kuzuia vifo vitokanavyo na watu kuzama maji.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la EMEDO, Editrudith Lukanga amesema shirika hilo limekuwa likitoa elimu kwa jamii hasa wavuvi ili kuchukua tahadhari ikiwemo kuvaa jaketi okozi (life jackets) na kufuatilia taarifa za hali ya hewa kabla ya kuingia majini ili kuepuka vifo vitokanavyo na kuzama maji.
Naye Afisa Mradi wa Kuzuia Kuzama Maji kutoka Shirika la EMEDO, Urthur Mgema amesema takwimu kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha zaidi ya watu laki tatu duniani hupoteza maisha kila mwaka kutokana na kuzama maji hivyo msisitizo mkubwa unatolewa kwa jamii kuchukua tahadhari kwani kuzama maji kunazuilika.
Akifungua maadhimisho hayo kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Henry Mwaijega ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutekeleza afua zitakazosaidia kudhibiti ajali na vifo vitokanavyo na watu kuzama maji hasa katika Ziwa Victoria, ambalo ni kitovu cha shughuli za kijamii na kiuchumi mkoani Mwanza ikiwemo uvuvi, usafirishaji na utalii.
Kaulimbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu 2026 inahimiza wadau mbalimbali kuungana pamoja ili kuzuia vifo vitokanavyo na kuzama maji, ikisema "Tuungane Kuzuia Vifo Vitokanavyo na Kuzama Maji".
Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu, Henry Mwaijega.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la EMEDO, Donald Kasongi akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la EMEDO, Editrudith Lukanga (kushoto) na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la EMEDO, Donald Kasongi (kulia), wakiwa kwenye maadhimisho hayo.
Viongozi mbalimbali meza kuu wakiongozwa na Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu, Henry Mwaijega (katikati) aliyemuakilisha Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza.
Wadau mbalimbali wakiwa kwenye maadhimisho hayo.
Serikali imesema itaendelea kuimarisha juhudi za kuzuia ajali na vifo vinavyotokana na kuzama maji katika Ziwa Victoria kupitia elimu, ushirikiano wa wadau na utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Taifa wa Kuzuia Kuzama Maji wa miaka mitamo kuanzia mwaka 2026 hadi 2031.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Henry Mwaijega ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kuzuia Kuzama Maji Duniani yaliyofanyika Julai 25, 2026, alisema usalama majini ni muhimu kwa kuwa Ziwa Victoria ni tegemeo la uchumi kupitia uvuvi, usafiri, biashara na utalii.
Alisema pamoja na umuhimu wa ziwa hilo, bado ajali za majini zinaendelea kupoteza maisha ya wananchi, hivyo Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha usimamizi wa maafa na hatua za kulinda maisha ya wananchi.
Mwaijega alisema warsha hiyo imelenga kutathmini mafanikio ya programu za usalama majini, kubaini changamoto na kuweka mikakati itakayoongeza ufanisi wa utekelezaji kwa kushirikisha Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo.
Aidha alisisitiza umuhimu wa kuwekeza katika tafiti, ukusanyaji wa takwimu, elimu ya usalama majini, mafunzo ya uokoaji na matumizi sahihi ya vifaa vya kujinusuru ili kupunguza ajali na vifo vinavyotokana na kuzama maji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la EMEDO na waandaaji wa warsha hiyo, Editrudith Lukanga alisema katika kipindi cha miaka mitano ya utekelezaji wa mradi huo, taasisi imeendesha mafunzo kwa wavuvi, kuhamasisha matumizi ya makoti ya kuokoa maisha na kuimarisha ushirikiano wa wadau.
Alisema juhudi hizo zinalenga kuwafanya wavuvi waingie ziwani wakiwa na uelewa wa kutosha kuhusu usalama na hivyo kupunguza vifo vinavyotokana na ajali za majini.
Lukanga alisema hakuna taasisi inayoweza kumaliza tatizo la kuzama maji peke yake, hivyo tathmini ya pamoja na ushirikiano wa wadau wote ni muhimu katika kuboresha hatua za usalama na kuokoa maisha.
















No comments: