TANZANIA MGENI RASMI MAONESHO YA UFUGAJI NYUKI AFRIKA NCHINI ALGERIA
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe Mobhare Matinyi, akizungumza na vyombo vya habari vya Algeria wakati akitangaza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekubali mwaliko wa kuwa mgeni rasmi katika Maonesho ya Ufugaji wa Nyuki barani Afrika (Africa Bee Expo) yatakayofunguliwa jijini Algiers mnamo Septemba 3, 2026.
Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe Mobhare Matinyi, akizungumza na vyombo vya habari vya Algeria wakati akitangaza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekubali mwaliko wa kuwa mgeni rasmi katika Maonesho ya Ufugaji wa Nyuki barani Afrika (Africa Bee Expo) yatakayofunguliwa jijini Algiers mnamo Septemba 3, 2026.Bw. Fatah Benchouia, Mwenyekiti wa Maonesho ya Ufugaji wa Nyuki barani Afrika (Africa Bee Expo) ya mwaka 2026, akizungumza na vyombo vya habari vya Algeria wakati wa kuitangaza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mgeni rasmi.
***
Tanzania imekubali mwaliko wa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Maonesho ya Ufugaji wa Nyuki barani Afrika yatakayofanyika jijini Algiers, Algeria, tarehe 3-6 Septemba, 2026.
Akizunngumza na waandishi wa habari wa televisheni za Algeria kwenye Ubalozi wa Tanzania jijini Algiers, Balozi Mobhare Matinyi alisema Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, ndiye atakayefungua maonesho hayo kwa niaba ya serikali.
Balozi Matinyi alisema Mhe. Waziri Dkt. Kijaji atakuja Algeria akiongoza ujumbe wa maafisa waandamizi na wataalamu wa serikali pamoja na wadau kutoka sekta binafsi ya ufugaji wa nyuki na utengenezaji wa bidhaa za nyuki nchini.
Balozi Matinyi alisema serikali inaipa sekta ya ufugaji wa nyuki umuhimu wa kipekee kwani inaajiri watu wapatao milioni mbili nchini na huingiza dola za Marekani milioni 77.5 (shilingi bilioni 205) kwa mwaka kutokana na mauzo ya asali katika nchi mbalimbali duniani.
Akinukuu takwimu za serikali, Balozi Matinyi alisema Tanzania hivi sasa ni ya pili kwa uzalishaji asali barani Afrika na ya kumi duniani na bado ikijipanga zaidi ina uwezo wa kufikisha mizinga ya nyuki takribani milioni 9.2 yenye uwezo wa kuzalisha tani 138,000 za asali na tani 9,200 za nta kwa mwaka.
Awali Mwenyekiti wa taasisi ya Algeria inayoandaa maonesho hayo, Fatah Benchouia, aliwaambia waandishi wa habari kwamba mbali ya uhusiano mzuri uliopo baina ya Algeria na Tanzania, lakini pia sababu kuu ya kuipa Tanzania heshima hii ni mafanikio yake katika sekta ya ufugaji wa nyuki ambapo kwa mwaka huzalisha tani 34,000 za asali kulinganisha na Algeria inayozalisha tani 7,300.
Bw. Benchouia aliambatana na Mwenyekiti wa Baraza la Kisayansi la taasisi inayoandaa maonesho hayo, Dkt. Abdelmadjid Bouchareb, pamoja na Rais na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Biashara cha Dunia hapa Algeria, Bw. Ahmed Tibaoaoui.
Maonesho hayo maarufu kwa jina la Africa Bee Expo 2026, yanafanyika kwa mara ya nne hapa Algeria na Tanzania inatarajia kuonesha mafanikio yake katika sekta hii na kujifunza kutoka kwa wafugaji na wazalishaji wa bidhaa za nyuki wa nchi zingine.
Imetolewa na Ubalozi wa Tanzania,
Algiers, Julai 20, 2026.

No comments: