LIVE STREAM ADS

Header Ads

TANZANIA NI SALAMA, TUKO TAYARI KWA AFCON 2027 – KATAMBI

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Patrobas Katambi, amesema Tanzania iko salama na imejiandaa kikamilifu kuhakikisha maandalizi ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 pamoja na mchakato wa kuandaa mashindano hayo unafanyika katika mazingira ya amani, utulivu na usalama wa hali ya juu.

Mhe. Katambi ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesisitiza kuwa Serikali imeweka mikakati madhubuti kupitia vyombo vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha Tanzania inakuwa tayari kwa mafanikio ya AFCON 2027.

Ameeleza kuwa maandalizi hayo yanaenda sambamba na juhudi za Serikali kuhakikisha Tanzania inatimiza viwango vinavyohitajika kimataifa katika maeneo mbalimbali ikiwemo usalama, miundombinu, huduma na mazingira bora kwa wachezaji, viongozi, wageni na mashabiki.
Mhe. Katambi amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika kuimarisha uwezo wa vyombo vya ulinzi na usalama kupitia utoaji wa mafunzo ya weledi, ununuzi wa vitendea kazi vya kisasa pamoja na matumizi ya teknolojia mpya za kiusalama.

Amesema Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeandaa mikakati maalumu ya kuhakikisha usalama wa AFCON 2027, ikiwemo mikakati 30 ya ndani na nje ya nchi, ambapo 15 ni ya wazi na 15 ni ya siri, kwa lengo la kuimarisha ulinzi na kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiusalama.

"Tanzania iko salama na tumejipanga kuhakikisha AFCON 2027 inafanyika katika mazingira ya amani na usalama. Vyombo vyetu vimejiandaa kimkakati, kimedani na kiteknolojia kuhakikisha washiriki na wageni wote wanakuwa salama," amesema Katambi.

Amesema katika kipindi cha maandalizi ya mashindano hayo, vyombo vya ulinzi na usalama vitaendelea kuimarisha ulinzi katika maeneo muhimu yakiwemo viwanja vya michezo, maeneo ya mazoezi, hoteli zitakazotumiwa na timu, viwanja vya ndege na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya watu.

Aidha, amesema kutakuwa na mifumo maalumu ya ukaguzi katika maeneo ya kuingia na kutoka ili kuhakikisha usalama wa wachezaji, viongozi wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), mashabiki na wageni mbalimbali.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, Serikali itaendelea kutumia mifumo ya kisasa ya kiintelijensia katika ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa ili kubaini mapema vitisho vinavyoweza kujitokeza, ikiwemo ugaidi, uhalifu wa mtandaoni, wizi na vurugu za mashabiki.

Ameongeza kuwa teknolojia mbalimbali zitatumika katika kuongeza ufanisi wa ulinzi, ikiwemo kamera za ufuatiliaji (CCTV), mifumo ya utambuzi wa wahusika, vifaa vya mawasiliano na mifumo ya kisasa ya ufuatiliaji.

Mhe. Katambi amesema Serikali pia imejipanga kuhakikisha usalama wa wachezaji, waamuzi, viongozi wa CAF, wageni wa heshima na mashabiki kutoka ndani na nje ya nchi kwa kuwawekea mazingira salama wakati wote wa mashindano.

Amesema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya vitendo vyovyote vinavyoweza kuvuruga maandalizi au utekelezaji wa AFCON 2027, ikiwemo wizi, ulanguzi wa tiketi, biashara haramu, matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vingine vya uvunjifu wa sheria.

Aidha, amesema Serikali imeandaa mipango ya kukabiliana na majanga mbalimbali ikiwemo moto, dharura za kiafya na matukio mengine yasiyotarajiwa, huku vikosi vya uokoaji na huduma za kwanza vikiandaliwa kwa ajili ya maeneo yote muhimu.
Ameeleza kuwa Tanzania itaendelea kuzingatia miongozo ya CAF pamoja na viwango vya kimataifa vya usalama wa mashindano makubwa ya michezo, ikiwa sehemu ya maandalizi kupitia Pamoja Bid ya kuwania uenyeji wa AFCON 2027.

Vilevile, Katambi amesema Tanzania itatumia uzoefu mbalimbali wa kimataifa katika kuboresha maandalizi yake, ikiwemo uzoefu alioupata wakati wa ziara yake nchini Marekani kuhusu maandalizi ya Kombe la Dunia 2026 katika maeneo ya tathmini ya vihatarishi, uratibu wa taasisi na mipango ya dharura.

Ameongeza kuwa mafanikio ya maandalizi na usalama wa AFCON 2027 yatategemea ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, vyombo vya ulinzi na usalama, waandaaji wa mashindano, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla.

Aidha, amewataka Watanzania kuendelea kudumisha amani na kupuuza taarifa au kampeni zinazolenga kuichafua Tanzania kupitia mitandao ya kijamii, akisema Serikali itaendelea kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama na yenye mazingira rafiki kwa uwekezaji, michezo na maendeleo.

No comments:

Powered by Blogger.