LIVE STREAM ADS

Header Ads

SERIKALI YAHIMIZA ELIMU ZAIDI KUDHIBITI MATUKIO YA WATU KUZAMA MAJI

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema matukio ya watu kuzama maji yanaweza kudhibitiwa ikiwa elimu, sera madhubuti na ushirikiano wa viongozi na wadau watashirikiana pamoja kutoa elimu kwa kuchukua hatua za kujilinda ikiwemo kuvaa mavazi okozi (life jackets) kabla ya kuingia majini.

Ujumbe huo wa Mkuu wa Mkoa Mtanda ulitolewa Jumanne Julai 28, 2026 na Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Christopher Ngubiagai wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kuzuia Kuzama Maji yaliyofanyika katika ufukwe wa Kamanga jijini Mwanza.

Alisema hali halisi inaonyesha kuwa wavuvi na watumiaji wa vyombo vya usafiri wa majini katika Ziwa Victoria wako hatarini zaidi dhidi ya ajali za kuzama maji kutokana na kutofuata kanuni za usalama kama kutumia vifaa vya kujiokoa na kufuatilia taarifa za utabiri wa hali ya hewa.

Alibainisha kuwa takwimu za mwaka 2024 / 2025 zinaonyesha kulikuwa na ajali 16 za majini katika Ziwa Victoria zilizohusisha watu 131 ambapo watu 21 walifariki dunia, sita walipotea na huku 104 wakiokolewa.

Kutokana na hali hiyo, alisema Serikali imeandaa Mpango Kazi wa Taifa wa Kuzuia Kuzama Maji wa miaka mitano (2026/ 2031), unaolenga kuimarisha uratibu wa wadau, kuongeza elimu kwa jamii pamoja na kuboresha hatua za kinga na uokoaji ili kupunguza vifo vinavyotokana na ajali za majini.

Kwa upande wake Editrudith Lukanga ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la EMEDO lililoandaa maadhimisho hayo alisema, zaidi ya watu 2,500 nchini hufariki kwa kuzama maji kila mwaka, huku asilimia 84 hadi 87 wakiwa watu wazima hususani wavuvi huku kidunia takwimu zikifikia zaidi ya watu laki tatu kila mwaka.

Lukanga alisema shirika la EMEDO litaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau mbalimbali kutoa elimi kwa jamii kuchukua hatua za kiusalama majini huku pia likisisitiza masuala ya kuzuia vifo vya kuzama maji kuingizwa katika mkakati wa uvuvi mdogo ili kuongeza usalama na kuokoa maisha ya wavuvi.

Siku ya kimataifa ya kuzuia kuzama maji hufanyika kila mwaka Julai 25 ambapo kwa mwaka huu 2026 maadhimisho hayo yameambatana na kaulimbiu isemayo, "Tuungane Kuzuia Vifo Vitokanavyo na Kuzama Maji".
Na George Binagi, BMG
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Christopher Ngubiagai.
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la EMEDO, Editrudith Lukanga.
Mkurugenzi Mtendaji Shirika la EMEDO, Editrudith Lukanga.
Wadau mbalimbali wakiwa kwenye maadhimisho hayo.
Wadau wakiwa kwenye maadhimisho hayo yaliyoambatana na utoaji elimu kwa wananchi.
Burudaji ya ngoma za asili ikiwa ni sehemu ya kutoa elimu kwa jamii.

No comments:

Powered by Blogger.