LIVE STREAM ADS

Header Ads

BODI YA NNE YA UENDESHAJI TICD YAANZA KAZI RASMI

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Bodi ya Nne ya Uendeshaji ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD), Ijumaa Agosti 07, 2026 imeanza rasmi kutekeleza majukumu yake baada ya kuapishwa na kufanya kikao chake cha kwanza.

Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Dkt. Rosemarie Mwaipopo, kampasi kuu ya Tengeru mkoani Arusha, kikiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Dkt. John Elton Lusingu.

Kikao hichi pia kimehudhuriwa na Katibu wa Bodi ambaye ni Mkuu wa Chuo cha TICD, Prof. Bakari George pamoja na wajumbe wa bodi ambao ni Dkt. Waheeda Shokat, Dkt. Alex Nkondola, Bw. Yasin Sanuku, Bw. Bahati Ndoweka na Bw. Martin Mashaka.

Awali kabla ya kuanza kwa kikao hicho wajumbe wa Bodi waliapishwa na kamishna wa viapo, Wakili Dunstan Shimbo ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Sheria TICD.

Kuapishwa na kuanza kwa shughuli za Bodi hiyo kunaiweka TICD katika nafasi mpya ya kuimarisha usimamizi wa kimkakati, kuongeza ubora wa elimu na mafunzo, kuimarisha tafiti na ubunifu.

Kupitia uongozi wa Bodi hiyo mpya, TICD inatarajia kuharakisha utekelezaji wa vipaumbele vya maendeleo ya Chuo, kuongeza ushindani wa kitaaluma na kuendelea kujijengea nafasi kama kitovu cha umahiri katika elimu ya maendeleo ya jamii nchini na Kanda ya Afrika Mashariki na Kati.

Kikao hicho pia kimehudhuriwa na mameneja kampasi kutoka kampasi zote nane za Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD) ambapo awali vilikuwa vyuo vya maendeleo ya jamii ufundi lakini kufuatia mabadiliko yaliyofanywa na Serikali, sasa vimekuwa kampasi za TICD.

Mabadiliko hayo yameanza Julai Mosi 2026 ambapo kampasi hizo ni TICD Misungwi, TICD Buhare, TICD Mlale, TICD Rungemba, TICD Monduli, TICD Uyole, TICD Mabughai na TICD Ruaha.
Mwenyekiti wa Bodi ya Nne ya Uendeshaji TICD- Dkt. John Elton Lusingu (kushoto) na Mkuu wa TICD- Prof. Bakari George (kulia), wakila kiapo cha kuanza rasmi majukumu yao.
Wajumbe wa Bodi ya Nne ya Uendeshaji TICD wakila kiapo cha kuanza rasmi majukumu yao.
Mkuu wa TICD- Prof. Bakari George (kulia) na Mwenyekiti wa Bodi ya Nne ya Uendeshaji TICD- Dkt. John Elton Lusingu (kushoto).
Mjumbe wa Bodi ya Nne ya Uendeshaji Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru (TICD), Yassin Ally.
Tazama VIDEO hapa chini Waziri Gwajima akizindua Bodi ya Nne ya TICD

No comments:

Powered by Blogger.