LIVE STREAM ADS

Header Ads

MWENGE WA UHURU WAZINDUA TAWI LA CRDB TINDE

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com

Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Tawi la Benki ya CRDB Tinde mkoani Shinyanga wakati wa uzinduzi rasmi wa tawi hilo.
Mwenge wa Uhuru ukiwa katika Tawi la Benki ya CRDB Tinde mkoani Shinyanga wakati wa uzinduzi rasmi wa tawi hilo.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang’onda, akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Tawi la Benki ya CRDB Tinde mkoani Shinyanga.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang’onda, akiwa pamoja na viongozi mbalimbali wakifurahia wakati wa uzinduzi wa Tawi la Benki ya CRDB Tinde mkoani Shinyanga.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang’onda, akitembelea Tawi la Benki ya CRDB Tinde mkoani Shinyanga wakati wa uzinduzi rasmi wa tawi hilo.
Mkurugenzi wa Mikopo wa Benki ya CRDB, Xavery Makwi, akiimba shairi wakati wa uzinduzi wa Tawi la Benki ya CRDB Tinde mkoani Shinyanga.
Mkurugenzi wa Mikopo wa Benki ya CRDB, Xavery Makwi, akiwa ameshika Mwenge wa Uhuru wakati wa uzinduzi wa Tawi la Benki ya CRDB Tinde mkoani Shinyanga.
Meneja wa CRDB Kanda ya Magharibi, Jumanne Wagana, akiwa ameshika Mwenge wa Uhuru wakati wa uzinduzi wa Tawi la Benki ya CRDB Tinde mkoani Shinyanga.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Azza Hillal Hamad, akiwa ameshika Mwenge wa Uhuru wakati wa uzinduzi wa Tawi la Benki ya CRDB Tinde mkoani Shinyanga.
Mwenge wa Uhuru ukiondoka katika Tawi la Benki ya CRDB Tinde mkoani Shinyanga baada ya kukamilika kwa shughuli za uzinduzi wa tawi hilo.


Mwenge wa Uhuru ukiondoka katika Tawi la Benki ya CRDB Tinde mkoani Shinyanga baada ya kukamilika kwa shughuli za uzinduzi wa tawi hilo.
Wafanyakazi wa Tawi la Benki ya CRDB Tinde mkoani Shinyanga.

Na Elizabeth Cosmas na Kadama Malunde - Shinyanga

Mwenge wa Uhuru umezindua rasmi Tawi la Benki ya CRDB Tinde mkoani Shinyanga, huku Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Wazo Michael Mwang’onda, akiipongeza benki hiyo kwa kuendelea kupanua wigo wa huduma za kifedha na kuzisogeza karibu na wananchi.

Tawi hilo lililopo Njiapanda ya Tinde, Kitongoji cha Uswahili, Kijiji cha Jomu, Wilaya ya Shinyanga, takribani kilomita 35 kutoka Shinyanga Mjini, limezinduliwa leo Alhamisi, Agosti 20, 2026, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa CRDB kuimarisha upatikanaji wa huduma za kifedha na kuboresha mazingira ya utoaji huduma kwa wateja.

Akizungumza mara baada ya kuzindua tawi hilo, Mwang’onda ameipongeza CRDB kwa kuendelea kutambua mahitaji ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini na kuchukua hatua za kuyafanyia kazi kwa kuwekeza katika miundombinu na huduma za kifedha.

“Nipende kuipongeza benki ya CRDB kwa kuendelea kupanua wigo wa huduma zake na kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali nchini. Leo tupo hapa kushuhudia uzinduzi wa tawi jingine la benki hii katika eneo la Tinde, hatua inayoonesha namna benki hii inavyotambua mahitaji ya wananchi na kuyafanyia kazi,” amesema Mwang’onda.
Amesema CRDB imeendelea kuwa kinara katika kuwahudumia Watanzania kwa kutambua mahitaji ya wananchi katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Tinde, na kuchukua hatua za kusogeza huduma za kifedha hadi maeneo ya vijijini.

“Benki ya CRDB imekuwa kinara katika kuwahudumia wananchi wa Tanzania. Ukiangalia mpaka sasa, CRDB imeona uhitaji wa wananchi wa Tinde na maeneo ya jirani na leo tuko hapa kuzindua tawi jipya kwa ajili ya kutoa huduma za kifedha,” amesema.

Mwang’onda amesema hatua hiyo haijaishia katika kufungua matawi pekee, bali CRDB imeendelea kuwekeza katika miundombinu na kusogeza huduma za kifedha karibu na wananchi, hatua inayolenga kuwawezesha kupata huduma hizo kwa urahisi na kuboresha mazingira ya utoaji huduma.

Aidha, Mwang’onda ameipongeza CRDB kwa namna inavyoshirikiana na Serikali katika utekelezaji wa programu mbalimbali zinazolenga kuwawezesha wananchi kiuchumi.
“Kati ya benki ambazo zinafanya kazi vyema na Serikali ni Benki ya CRDB. Fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya makundi maalumu kwa lengo la kuwawezesha kiuchumi zinapita katika benki hii,” amesema.

Ameongeza kuwa Benki ya CRDB pia inashiriki katika udhamini wa Michezo na utoaji wa mikopo inayolenga kuwawezesha vijana kiuchumi, akisema ushiriki huo unaonesha uwezo na umahiri wa benki hii katika kutoa huduma kwa wananchi.

“Pamoja na mikopo inayotolewa kwa ajili ya kuwawezesha vijana kiuchumi, zaidi ya milioni 200, CRDB inahusika pia. Hii inaonesha umahiri wa utendaji kazi katika benki yenu, hivyo niwapongeze sana,” amesema.

Mwang’onda ameitaka Benki ya CRDB kuendelea kupanua huduma zake na kuwafikia wananchi wengi zaidi ili kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
“Na niendelee tu kuwapongeza na zaidi ya yote, nawasihi kuendelea kuwahudumia wananchi wenu ili kuhakikisha kila Mtanzania anainuka kiuchumi,” amesema.

Aidha, ametoa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji katika sekta ya fedha, jambo linaloiwezesha CRDB kuendelea kupanua huduma na kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mikopo wa CRDB, Xavery Makwi, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Dkt. Abdulmajid Mussa Nsekela, amewataka wananchi wa Tinde na maeneo jirani kutumia fursa za mikopo na huduma za kifedha zinazotolewa na benki hiyo.
Amesema CRDB imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi trilioni 31 kwa makundi mbalimbali, yakiwemo wakulima, wafanyabiashara, watumishi, wastaafu na watu binafsi, huku akisisitiza kuwa uwepo wa tawi hilo utawawezesha wananchi kupata huduma bila kusafiri hadi Shinyanga Mjini.

Makwi amesema Tawi la Tinde ni miongoni mwa matawi 25 ya CRDB katika Kanda ya Magharibi, inayojumuisha Shinyanga, Tabora, Kigoma na Geita.

Ameongeza kuwa ujenzi wa tawi hilo umegharimu shilingi milioni 650, zilizotumika katika ununuzi wa ardhi, ujenzi wa jengo na uwekaji wa vifaa, huku tawi hilo likihamia katika jengo jipya Aprili 2026.
Kwa upande wao, wananchi wa Tinde wameishukuru Benki ya CRDB kwa kuwasogezea huduma za kifedha karibu na maeneo yao, wakisema uwepo wa tawi hilo utawarahisishia kupata huduma za kibenki bila kulazimika kusafiri hadi Shinyanga Mjini.

Wamesema awali walilazimika kutumia muda na gharama za usafiri kwenda Shinyanga mjini kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali za kibenki, ikiwemo kuweka na kutoa fedha, lakini uwepo wa tawi hilo Tinde umewaondolea changamoto hiyo.

Wamesema hatua hiyo pia itaongeza urahisi na usalama katika matumizi ya huduma za kifedha, huku wakiitaja kuwa fursa muhimu kwa wakazi wa Tinde na maeneo jirani katika kukuza shughuli zao za kiuchumi.


TAZAMA PICHA ZAIDI HAPA

No comments:

Powered by Blogger.