“NIMEBEBA USHUHUDA” KULIPAMBA TAMASHA KUBWA LA KVC SHINYANGA
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mwenyekiti wa Kambarage Vijana Choir, Heri Ndaki, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Tamasha la Uimbaji Mubashara ‘Nimebeba Ushuhuda’ linalotarajiwa kufanyika Oktoba 16, 2026 katika Kanisa la AIC Kambarage, Manispaa ya Shinyanga.
Na Elizabeth Cosmas - Shinyanga
Kwaya ya Vijana ya Kanisa la AIC Kambarage, maarufu kama Kambarage Vijana Choir (KVC), imeandaa Tamasha la Uimbaji Mubashara litakalobeba jina la “Nimebeba Ushuhuda”, huku likilenga kuunganisha waumini wa madhehebu mbalimbali na kuhamasisha jamii kudumisha amani, upendo na mshikamano.
Tamasha hilo linatarajiwa kufanyika Oktoba 16, 2026 katika Kanisa la AIC Kambarage, Manispaa ya Shinyanga, ambapo KVC imerekodi nyimbo 15 za Injili zitakazounda albamu hiyo mpya.
Akizungumza leo, Agosti 22, 2026, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Mjini Shinyanga, Mwenyekiti wa Kambarage Vijana Choir, Heri Ndaki, amesema tamasha hilo ni sehemu ya mpango wa kwaya kutumia muziki wa Injili kuifikia jamii na kutoa ujumbe wa upendo, amani na kuwajali wenye mahitaji.
Ndaki amesema pamoja na maandalizi ya tamasha hilo, KVC imejipanga kufanya shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo kuwasaidia wafungwa, wazee na watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
“Tutakuwa na shughuli za kutoa msaada kwa jamii kabla ya tukio kwa watu wenye mahitaji maalum ndani ya Manispaa ya Shinyanga. Tunataka kudumisha fikra za vijana za kusaidia jamii zao kwa akili, nguvu na rasilimali zao, na huku ndiko kumhubiri Kristo,” amesema Ndaki.
Amesema ni muhimu kwa viongozi wa dini na waumini kutoka madhehebu mbalimbali kuendelea kuungana katika kuliombea Taifa na kuhamasisha amani, upendo na mshikamano ndani ya jamii.
Ndaki ameongeza kuwa jamii inapaswa kushirikiana kukemea vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, akisisitiza kuwa vijana wana nafasi kubwa ya kuwa sehemu ya suluhisho kwa kutumia vipaji, nguvu na uwezo wao kuleta mabadiliko chanya.
Kwa upande wake, Mchungaji wa Kanisa la AIC Kambarage, Mapambano Jacob, amesema kanisa limeendelea kuwalea vijana kupitia vipaji mbalimbali, ikiwemo muziki, ili kuwajenga kuwa watu wenye maadili na uwezo wa kushiriki katika kujenga Taifa.
Mchungaji Jacob amesema Kambarage Vijana Choir ilianzishwa mwaka 1995 na kwamba kwa kipindi chote hicho imeendelea kusimamiwa na kulelewa na kanisa, hatua iliyoiwezesha kufikia hatua ya kuandaa albamu yenye nyimbo 15.
Amesema vijana wana mchango mkubwa katika kuamua mustakabali wa Taifa, hususan katika kuimarisha amani, umoja na mshikamano.
“Taifa letu lina amani na limewapa vijana nafasi ya kufanya shughuli hii ya uimbaji. Tunashukuru Serikali inayoongozwa na Dk. Samia kwa kuendelea kusimamia amani,” amesema Mchungaji Jacob.
Ameeleza kuwa amani iliyopo nchini imekuwa mazingira muhimu yanayowawezesha vijana kufanya shughuli mbalimbali, ikiwemo uimbaji wa Injili, huku akiwataka waumini wa madhehebu mbalimbali kutumia fursa hiyo kuungana na kuombea Taifa.
Naye Mwenyekiti wa Habari na Mawasiliano kwa Umma wa KVC, Reuben Emmanuel, amesema tamasha hilo litakuwa na uimbaji mubashara wa nyimbo zote 15 zinazounda albamu ya Nimebeba Ushuhuda.

Emmanuel amesema KVC pia itauza mavazi yenye chapa na ujumbe wa albamu hiyo kwa bei ya kuanzia Shilingi 10,000 hadi Shilingi 25,000, kutegemea aina na ukubwa wa vazi kwa watu wazima na watoto.
Ameomba wadau mbalimbali kuendelea kuunga mkono maandalizi ya tamasha hilo kwa kuchangia kupitia M-Pesa namba 58130016 au akaunti ya CRDB, AIC KVC Maendeleo, namba 0133583913800.
Wadau wanaotaka kupata maelezo zaidi kuhusu tamasha hilo wanaweza kuwasiliana na KVC kupitia namba 0752-265721 au 0627-265721.
Kwa mujibu wa waandaaji, baadhi ya wadhamini ambao tayari wameunga mkono shughuli hiyo ni Jambo FM, Vigmark Hotel na Chuo cha Sayansi ya Afya Kolandoto.
KVC imewaalika waumini na wananchi kutoka Shinyanga na maeneo mbalimbali nchini kushiriki katika tamasha hilo la Live Recording, huku ikisisitiza kuwa muziki wa Injili utatumika kama nyenzo ya kuhubiri upendo, amani, maadili mema na mshikamano katika jamii.
Kwaya hiyo inatumia kaulimbiu “KVC, Ulimwengu Unasikiliza Injili.”






































No comments: