LIVE STREAM ADS

Header Ads

TanTrade yafungua fursa ya soko la Afrika Mashariki kwa wafanyabiashara wa Tanzania

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mikoa sita ya Kanda ya Ziwa imechangia shilingi trilioni 54.4, sawa na asilimia 23 ya Pato la Taifa (GDP) kwa mwaka uliopita, huku Mkoa wa Mwanza ukiongoza kwa kuchangia shilingi trilioni 14.7 sawa na asilimia 7.2 ya Pato la Taifa.

Takwimu hizo zimetolewa Alhamisi Septemba 03, 2026 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kuendeleza Biashara Tanzania (TanTrade), Ephraim Mafuru wakati akizungumza na waandishi wa habari katika banda la TanTrade kwenye Maonesho ya 21 ya Biashara ya Afrika Mashariki yanayoendelea katika Uwanja wa Furahisha, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza.

Maonesho hayo yameandaliwa na Chemba ya Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Mwanza.

Mafuru alisema takwimu hizo zinaonesha umuhimu mkubwa wa Kanda ya Ziwa katika uzalishaji wa bidhaa mbalimbali na mchango wake katika uchumi wa Taifa, hivyo maonesho hayo kuwa fursa muhimu kwa wafanyabiashara wa Tanzania kuunganishwa na masoko ya Afrika Mashariki.

Alisema Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ina soko la watu takribani milioni 507, ambalo linatoa fursa kubwa kwa wazalishaji, wafanyabiashara na wasambazaji wa bidhaa zinazozalishwa nchini.

Kwa mujibu wa Mafuru, zaidi ya waoneshaji 250 wameshiriki katika maonesho hayo huku TanTrade ikiendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuhakikisha wafanyabiashara wanapata masoko ndani na nje ya Tanzania.

“Kazi ya TanTrade si Maonesho ya Sabasaba pekee jijini Dar es Salaam. Kazi yetu ni ndani na nje ya nchi, na hapa tunakutana na wateja wengi kutoka katika Jumuiya nzima ya Afrika Mashariki” alisema Mafuru.

Alisema TanTrade inajivunia kushirikiana na wafanyabiashara, hususan TCCIA Mkoa wa Mwanza, ambayo imefanya kazi kubwa ya kuwaunganisha wazalishaji na fursa za kushiriki katika maonesho hayo.
‘Made in Tanzania’ muhimu kufungua masoko
Mafuru alisisitiza umuhimu wa wafanyabiashara kuhakikisha bidhaa zao zina ubora na zinakuwa na nembo ya “Made in Tanzania”, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kuthibitisha uhalisia na ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini.

Alisema bidhaa zinazopitia uthibitisho wa taasisi kama Shirika la Viwango Tanzania (TBS) zinapaswa kuwa na ubora unaokidhi viwango, akieleza kuwa uthibitisho huo unatambulika Tanzania, katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na ndani ya Jumuiya ya Afrika.

Aidha aliwataka watanzania kutumia fursa zilizopo kuongeza uzalishaji na kipato, badala ya kuzungumzia fursa bila kuchukua hatua za kuzitumia.

“Tusiziimbe fursa pekee yake. Tuna maziwa makubwa, tuna ardhi, tuna mito; je, umefanya nini? Fanya kazi, ongeza kipato chako mmoja mmoja na Taifa” alisema.
Kanda ya Ziwa yatakiwa kuongeza thamani ya bidhaa

Mafuru alisema hakuna maana ya kuwa na fursa nyingi bila kuzalisha bidhaa zenye ubora, kuongeza thamani na kuzifikisha katika masoko yenye uwezo wa kutoa faida kwa wazalishaji.

Alitoa mfano wa sekta ya madini, akisema Kanda ya Ziwa inaongoza katika uzalishaji wa dhahabu, ikiwemo Mkoa wa Geita, lakini bado baadhi ya maeneo yanaendelea kutegemea bidhaa nyingi kutoka nje ya nchi.

Alitolea mfano wa Katoro, akisema takribani asilimia 90 ya bidhaa zinazotumika katika eneo hilo, bila kuhusisha chakula, zinatoka nje.

Kwa msingi huo, alisisitiza umuhimu wa kuwawezesha Watanzania kuongeza uzalishaji wa bidhaa kwa wingi na ubora ili waweze kushindana katika masoko ya kimataifa.

Pia alizitaka taasisi za Serikali kubadili mtazamo kutoka kuwa wadhibiti pekee na badala yake kuongeza juhudi za kuwawezesha wafanyabiashara na wazalishaji kukua. 
Wafanyabiashara wa Uganda wanufaika
Kwa upande wake, Meneja wa Huduma kwa Wateja wa kampuni ya Proofings kutoka Uganda, Kigozi Henry alisema kampuni hiyo imekuwa ikishiriki katika maonesho hayo kila mwaka, ikiwa inajihusisha na utengenezaji wa bidhaa za ujenzi.

Kigozi alipongeza ushirikiano uliopo kati ya TanTrade na TCCIA, akisema umewapa fursa ya kuonesha bidhaa zao na kuwafikia wateja nchini Tanzania.

Naye mjasiriamali aliyeshiriki katika maonesho hayo, Mercy Ntabago aliwataka wakulima na wazalishaji wa bidhaa asilia kutumia fursa zinazotolewa na TanTrade.

Alisema TanTrade imekuwa ikiwapatia elimu, kuwaunganisha na masoko na kuwasaidia kuvuka mipaka ya Tanzania kwa kuwezesha bidhaa zao kuwa na nembo ya “Made in Tanzania.”

Maonesho ya 21 ya Biashara ya Afrika Mashariki yamelenga kuwaunganisha wazalishaji, wafanyabiashara na wanunuzi kutoka Tanzania na nchi za Afrika Mashariki na Kati

No comments:

Powered by Blogger.