LIVE STREAM ADS

Header Ads

JAMII YAHIMIZWA KUTENGA MUDA WA KUFUATILIA MALEZI YA WATOTO

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Wazazi na walezi nchini wamehimizwa kuwa na muda wa kufuatiliaji malezi ya watoto wao, hatua itakayosaidia kubaini mapema changamoto zinazowakabili na kuchukua za kuzitafutia ufumbuzi.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Amina Makilangi ametoa rai hiyo wakati akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dkt. Dorothy Gwajima kwenye mbio za Mtoto ni Malezi Fun Run zilizofanyika uwanja wa CCM Kirumba ili kuhamasisha malezi chanya katika jamii.

Amesema malezi hayaishii katika kuwapatia watoto mahitaji ya msingi pekee, bali yanahitaji wazazi kuwa karibu nao, kuwasikiliza na kuwapa mwongozo unaowasaidia kukua katika misingi ya maadili.

Amesema wazazi na walezi wanapaswa kuhakikisha watoto wanapata upendo, ulinzi, elimu na malezi yenye maadili, huku wakifuatilia kwa karibu mambo yanayoweza kuathiri maisha na maendeleo yao badala ya kujikita kwenye shughuli za kutafuta tu kipato na kuacha jukumu la malezi kwa wasaidizi wa watoto.
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Compassion International Tanzania, Mary Lema amesema mbio hizo pia zililenga kutumia michezo kama njia ya kuwahamasisha wazazi kutumia muda wao pamoja na watoto.

Lema amesema kushiriki michezo na shughuli nyingine za kijamii pamoja na watoto kunaweza kusaidia kuimarisha mawasiliano ndani ya familia na kujenga uhusiano mzuri kati ya wazazi na watoto.

Baadhi ya wazazi na watoto walioshiriki mbio hizo wakiwemo Mohamedi Badru na Lucia Lawrence wamesema mbio hizo zimeongeza hamasa ya wazazi na walezi kuwa karibu na watoto wao hatua ambayo itasaidia kuimarisha uhusiano wa kifamilia.

Wamesema mbio hizo zina nafasi ya kuwakutanisha wazazi na watoto katika mazingira yasiyo rasmi, hivyo kutoa fursa ya kuzungumza, kucheza na kufahamiana zaidi.

Mbio hizo zimeandaliwa kwa ushirikiano wa Serikali na wadau wakiwemo Shirika la Compassion International Tanzania, SOS Children's Village Tanzania na TECD zikilenga kuhamasisha malezi chaja ya watoto katika jamii.

No comments:

Powered by Blogger.