WAZAZI, WALEZI WAHIMIZA KUIMARISHA MALEZI BORA KWA WATOTO
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mabadiliko ya maisha na kuongezeka kwa majukumu ya kila siku kwa wazazi na walezi katika jamii, yameelezwa kuwa miongoni mwa changamoto zinazoathiri malezi na ufuatiliaji wa watoto, huku wadau wakisisitiza umuhimu wa jamii kuchukua hatua katika kulinda maadili na ustawi wa watoto.
Hayo yamejiri Ijumaa Septemba 04, 2026 jijini Mwanza wakati wa kongamano la Mtoto ni Malezi lililowakutanisha pamoja wadau wadau mbalimbalu kwa lengo la kutafuta namna bora ya kuimarisha malezi na makuzi ya watoto nchini.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza- Dkt. Silas Wambura amesema uzoefu wa wadau una nafasi kubwa katika kubaini changamoto zinazojitokeza wakati wa utekelezaji wa mikakati ya Serikali.
Dkt. Wambura amesema Serikali tayari imeweka mifumo mbalimbali inayolenga kuimarisha malezi na makuzi ya watoto, lakini utekelezaji wake unahitaji tathmini endelevu ili kubaini maeneo yanayohitaji maboresho.
Amesema maoni kutoka kwa wadau yatasaidia Serikali kufanya marekebisho pale yanapohitajika na kuhakikisha sera pamoja na mikakati ijayo inaendana na mahitaji halisi ya watoto na jamii.
“Tunapoenda kwenye mjadala huu mtaangalia mikakati ambayo tumeweka kama Serikali ili mtushauri namna gani ya kuboresha” amesema Dkt. Wambura.
Afisa Tarafa ya Ilemela, James Chuwa akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amiri Mkalipa amesema suala la muda limekuwa changamoto kwa baadhi ya wazazi kutokana na majukumu mbalimbali yanayowakabili yakiwemo ya kiuchumi.Chuwa amesema baadhi ya wazazi wanashindwa kutumia muda wa kutosha kuwa karibu na watoto wao, hali ambayo inaweza kupunguza ufuatiliaji wa mienendo yao na kuwafanya wazazi kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu changamoto zinazowakabili watoto.
Amesisitiza umuhimu wa wazazi kutenga muda kwa ajili ya watoto licha ya majukumu mengine, kwa kuwa ukaribu wa mzazi na mtoto ni sehemu muhimu ya malezi.
Baadhi ya viongozi wa dini walioshiriki kongamano hilo wameeleza wasiwasi wao kuhusu hali ya malezi katika jamii, wakisema suala hilo lisipopewa uzito unaostahili linaweza kuwa na athari kwa kizazi kijacho.
Askofu Mkuu wa AICT, Mussa Magwesela amesema suala la malezi halipaswi kuachwa kuwa jukumu la mzazi pekee, bali linahitaji ushirikiano wa familia, Serikali, viongozi wa dini na jamii kwa ujumla.
Askofu Magwesela ametahadharisha wazazi na walezi kuwa makini na kufuatilia malezi ya watoto kutokana na muingiliano wa teknolojia ambao unaweza kuharibu ukuaji wa watoto ikiwa watakosa uangalizi mzuri.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Compassion International Tanzania, Mary Lema amesema shirika hilo lina jumla ya 600 vya malezi ya watoto vinavyosimamiwa na makanisa mbalimbali katika Wilaya 91 nchini hivyo kupitia kongamano hilo, wadau watatoa mikakati itakayosaidia kuimarisha malezi ya watoto katika vituo hivyo na jamii kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miradi Shirika la SOS Children's Village Tanzania, John Fulli amesema malezi bora ni muhimu kwa ulinzi na ustawi wa watoto hivyo juhudi za kuimarisha malezi zinapaswa kutoishia kutoa tu elimu, bali pia kuimarisha ustawi wa familia kiuchumi, lishe bora pamoja na ulinzi na usalama kwa watoto.
Kongamano hilo ambalo ni sehemu ya kuelekea kwenye mbio za Mtoto ni Malezi Fun Run zitakazofanyika Jumamosi Septemba 05, 2026 katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, pia limejadili kuhusu umuhimu wa kuendelea kuzipitia sera na mikakati ya malezi ya waoto ili kuendana na changamoto za sasa zinazojitokeza katika jamii.



No comments: