LIVE STREAM ADS

Header Ads

WATENDAJI WATAKIWA KUZINGATIA HAKI, WAJIBU KATIKA KUHUDUMIA WANANCHI

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Wizara ya Katiba na Sheria imeendelea kuimarisha utoaji wa elimu ya uraia na utawala bora kwa viongozi na watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa katika Wilaya ya Babati, mkoani Manyara, kupitia mafunzo yanayolenga kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, misingi ya haki, uwajibikaji na utawala bora.

Akihitimisha mafunzo hayo wilayani Babati, Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Hamis Mgandilwa, amewataka viongozi na watendaji hao kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya haki, uwajibikaji, uadilifu na weledi ili kuhakikisha huduma za umma zinatolewa kwa usawa na kwa mujibu wa sheria.

Amesisitiza kuwa ni wajibu wa kila mtumishi wa umma kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki bila kubaguliwa, huku akiwahimiza kusimamia ipasavyo utekelezaji wa majukumu yao kwa maslahi ya wananchi na maendeleo ya jamii.

Mhe. Mgandilwa ameeleza kuwa uelewa wa sheria na misingi ya utawala bora ni muhimu katika kuwawezesha watumishi wa umma kufanya maamuzi sahihi, kusimamia haki za wananchi na kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa viongozi na watendaji kuwa karibu na wananchi, kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi kwa wakati ili kuimarisha imani ya wananchi kwa Serikali na taasisi zake.

Awali, akizungumza katika mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Katiba na Ufuatiliaji, Bi. Jane Lyimo, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha viongozi na watendaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kupata uelewa mpana kuhusu namna bora ya kutoa elimu ya uraia kwa wananchi, hususan kuhusu haki na wajibu wao, katika Kutenda haki kwa wananchi.

Aidha, Bi. Lyimo amesisitiza kuwa kila mwananchi anastahili kuhudumiwa bila kujali hali yake aliyonayo na kupewa thamani kwa hila huduma anayohitaji

Kupitia mafunzo hayo, viongozi na watendaji wanatarajiwa kutumia maarifa waliyoyapata katika kuboresha utoaji wa huduma, kuimarisha uwajibikaji na kujenga mazingira yanayoheshimu sheria, haki za wananchi na misingi ya utawala bora katika Wilaya ya Babati na maeneo mengine ya Mkoa wa Manyara.

No comments:

Powered by Blogger.