LIVE STREAM ADS

Header Ads

JAB YASISITIZA UZINGATIAJI WA MAADILI NA WELEDI KATIKA UANDISHI WA HABARI

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com

Na Mwandishi Wetu.

Wanafunzi wa uandishi wa habari wamehimizwa kutotosheka na elimu ya ngazi ya cheti au stashahada, bali waendelee kujiendeleza hadi kufikia ngazi za juu zaidi ili kujenga uwezo, weledi na ushindani katika taaluma hiyo.

Wito huo umetolewa tarehe 22 Oktoba, 2026, na Afisa Habari Mkuu kutoka Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB), Bw. Prudence Constantine, wakati wa ziara ya maafisa wa Bodi katika Chuo cha Uandishi wa Habari Dar es Salaam (Dar es Salaam School of Journalism-DSJ).

Ziara hiyo imelenga kujifunza kuhusu mazingira na mifumo ya utoaji wa mafunzo ya uandishi wa habari, kuimarisha ushirikiano kati ya JAB na chuo hicho, pamoja na kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanawaandaa wanafunzi kukidhi viwango vya elimu, ithibati, maadili na weledi vinavyohitajika katika taaluma ya uandishi wa habari.
Akizungumza na wanafunzi wanaosoma ngazi ya cheti, Constantine amesema taaluma ya uandishi wa habari inahitaji watu wenye elimu, ujuzi na maarifa mapana ili waweze kukabiliana na mabadiliko na changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao.

Amewataka wanafunzi hao kujikita katika masomo, kujenga utamaduni wa kujifunza na kuendelea kupanua maarifa yao, akieleza kuwa maendeleo ya teknolojia na mabadiliko katika tasnia ya habari yanahitaji Waandishi wa Habari wenye uwezo wa kuendana na wakati.

Katika mazungumzo hayo, maafisa wa JAB walikutana na wanafunzi na wakufunzi wa DSJ na kujadiliana kuhusu mafunzo, viwango vya taaluma na umuhimu wa kuimarisha mazingira ya ujifunzaji na kuwaandaa wanafunzi kutekeleza majukumu ya kihabari kwa kuzingatia weledi na maadili.
Kwa upande wao, wakufunzi wa DSJ wameiomba JAB kuendelea kutekeleza majukumu yake ya kusimamia na kuimarisha taaluma ya uandishi wa habari, ili kuhakikisha Waandishi wa Habari wanazingatia maadili, weledi na misingi ya taaluma hiyo.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za JAB za kuimarisha ushirikiano na vyuo vinavyotoa mafunzo ya uandishi wa habari, kwa lengo la kuboresha maandalizi ya wataalamu na kuinua viwango vya taaluma nchini.

No comments:

Powered by Blogger.