MHE. LONDO AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA TANZANIA NCHINI ETHIOPIA
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
📌Lengo ni kujadili fursa za kibiashara na uwekezaji nchini Ethiopia;
📌Balozi Shiyo aishukuru timu ya Tanzania kwa kupeperusha bendera ya nchi kwenye mkutano wa jukwaa la maendeleo ya kibiashara la Afrika.
Addis Ababa, Ethiopia.
Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo (Mb), amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia Mhe Balozi Innocent Shiyo Mara baada ya ushiriki wa Tanzania kwenye mkutano wa jukwaa la maendeleo ya biashara la Afrika nchini Ethiopia ambapo Tanzania ilishiriki pia.
Mhe Londo aliambatana na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Dkt Natu Mwamba na ujumbe wa wawakilishi kutoka Wizara ya viwanda ma biashara.
Mhe Londo amesema ni vema Tanzania ikatumia fursa za biashara za kikanda na kimataifa pamoja na ushirikiano na wadau wa maendeleo, Kama TradeMark Africa, kuimarisha mifumo ya biashara, kuongeza thamani na kiasi cha bidhaa zinazouzwa nje ya nchi.
Amesema Tanzania inaendelea kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi imara, jumuishi na shindani, huku biashara ikiwa miongoni mwa nyenzo muhimu za kufikia malengo hayo na kuongeza kuwa hadi Juni 2026, Tanzania ilikuwa imeuza nje bidhaa zenye thamani ya takribani Dola za Marekani bilioni 19.98, akibainisha kuwa kipaumbele ni kuongeza kiwango na thamani ya bidhaa hizo, ikiwemo kutumia fursa za Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia Mhe Innocent Shiyo amemshukuru Mhe Naibu Waziri na ujumbe wake kwa kuinadi vema nchi ya Tanzania kwenye mkutano huo ili kufungua fursa za kibiashara kwa Afrika na kutumia fursa kufanya biashara na Ethiopia.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Londo alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa viwanda na biashara na ushirika wa Uganda Mhe Sanjay Tenna na walijadili kwa pamoja namna ya kufanya biashara ya Michele na nchi ya Uganda na baadae kufanya mazungumzo na Katibu mkuu viwanda na biashara na utalii wa Burundi Christine Niragira kwa lengo la kuongeza fursa zaidi za biashara na uwekezaji kwa nchi hizo mbili sambamba na kuimarisha miundombinu ya kurahisisha biashara, hususan Bandari ya Kigoma na maeneo yanayounganisha Tanzania na nchi jirani, ili kuongeza mauzo katika masoko ya Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda na Uganda.
Akitolea mfano wa Burundi, amesema nchi hiyo iliagiza bidhaa zenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.31, ambapo Tanzania iliuza bidhaa zenye thamani ya Dola milioni 134 pekee, hali inayoonesha fursa kubwa ya kuongeza mauzo.








No comments: