WANAHABARI WATAKIWA KUZINGATIA WELEDI, USALAMA WAWAPO KAZINI
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Waandishi wa habari wametakiwa kuzingatia usalama wao pamoja na maadili ya taaluma wanapotekeleza majukumu yao, hatua inayowasaidia kuepuka migogoro inayoweza kuzuilika.
Wito huo umetolewa wakati wa mafunzo yaliyofanyika mkoani Tanga, yakiwashirikisha wanahabari kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kujilinda wanapotekeleza majukumu yao.
Mkufunzi wa mafunzo hayo, Raisa Said, ambaye ni Katibu Msaidizi wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Tanga (Tanga Press Club) na mwandishi wa habari wa Clouds TV, alielezea umuhimu wa waandishi kutambua vihatarishi vya usalama na kuchukua tahadhari zinazofaa ili kujilinda wanapokuwa kazini.
Mafunzo hayo yamefanyika wakati ambapo waandishi wa habari wanakabiliwa na changamoto mbalimbali wanapokusanya habari, ikiwemo namna ya kutekeleza majukumu yao katika mazingira nyeti, hasa wanapowasiliana na viongozi wa umma kuripoti masuala yanayoweza kuvuta hisia za taasisi mbalimbali.
Akiwahimiza waandishi hao kuongeza umakini wanapokabiliwa na mazingira yanayoweza kuwa na changamoto za kiusalama, Raisa alisema ni muhimu kuhakikisha kuwa mienendo na vitendo vyao haviwaweki katika hatari zinazoweza kuepukika.
Aidha mkufunzi huyo aliwataka wanahabari kuzingatia weledi, kuheshimu taratibu zilizowekwa na kuwa na mawasiliano mazuri na wadau wa habari, akieleza kuwa mambo hayo ni muhimu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Katika mafunzo hayo, Raisa pia aliwasisitiza waandishi wa habari kutambua wajibu unaoambatana na taaluma yao, hususan wanaporipoti masuala yanayohusu taasisi za umma na vyombo vya ulinzi na usalama.
Alidokeza kuwa usalama wa wanahabari ni jambo muhimu katika kuhakikisha vyombo vya habari vinaendelea kutekeleza wajibu wake wa kuhabarisha umma, pamoja na kufuatilia uwajibikaji wa viongozi na taasisi za umma.
Mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) kwa kushirikiana na IMS, yaliwashirikisha waandishi wa habari 21 mkoani Tanga, yakilenga kuwaongezea uelewa kuhusu usalama binafsi na mwenendo wa kitaaluma wanapokuwa kazini.



No comments: