TRA YASOGEZA HUDUMA ZA KODI KARIBU NA WANANCHI, VIKUNDI ZAIDI YA 50 VYASAJILIWA MOROGORO
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kuimarisha utoaji wa huduma na elimu ya kodi kwa wananchi kupitia Kliniki ya Kodi iliyofanyika kuanzia tarehe 9 hadi 14 Novemba 2026 katika maeneo ya Mlimba, Mugeta, Mbingu na Mahenge, Mkoa wa Morogoro.
Kliniki hiyo imelenga kuwafikia wafanyabiashara katika maeneo yao ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za kodi, ambapo zaidi ya vikundi 50 vya wafanyabiashara vimesajiliwa.
Katika ziara hiyo, Meneja wa Kituo cha TRA Mlimba, Bi. Loveness Mwakipesile, alishiriki kikamilifu katika utoaji wa huduma kwa walipakodi, ikiwemo kutoa elimu ya kodi, kusikiliza changamoto zao na kutoa ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali ya kodi.
Aidha, walipakodi wenye changamoto mbalimbali walipata huduma na msaada wa moja kwa moja kutoka kwa wataalamu wa TRA.
Usajili wa vikundi hivyo ni hatua inayochangia kupanua wigo wa walipakodi.
Wafanyabiashara walioshiriki katika Clinic hizo wameeleza kufurahishwa na huduma hizo, wakitoa shukrani kwa TRA kwa kuwafuata katika maeneo yao ya biashara na kuwasogezea huduma karibu na milango yao, badala ya wao kulazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hizo.
Wamesema utaratibu huo umewarahisishia kupata elimu, huduma na ufumbuzi wa changamoto zao za kikodi.
TRA inaendelea kutekeleza mpango wa Kliniki za Kodi kwa lengo la kuimarisha uhusiano na jamii ya wafanyabiashara, kuongeza uelewa wa masuala ya kodi na kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari kwa maendeleo endelevu ya Taifa.





No comments: