LIVE STREAM ADS

Header Ads

UKOSEFU WA TAARIFA WATAJWA CHANZO VIJANA KUKOSA FURSA

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Vijana wametakiwa kutafuta taarifa sahihi kupitia vyanzo rasmi kuhusu fursa mbalimbali zilizopo nchini ili waweze kunufaika nazo.

Rai hiyo imetolewa Novemba Ijumaa 13, 2026 na Afisa Maendeleo ya Vijana kutoka Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Michael Magesa wakati akizungumza na vijana kutoka mashirika mbalimbali walioshiriki warsha ya siku moja iliyoandaliwa na shirika la Power of Youth Development (PYD).

Alisema vijana wengi hutegemea taarifa za kusikia kutoka vyanzo vizivyo rasmi ambazo mara nyingi si sahihi hatua inayopelekea kushindwa kupata fursa na uwezeshwaji kikamilifu.

"Vijana mnakosa fursa kwa sababu hamtafuti taarifa za wapi fursa zilipo, na kama haupati taarifa huwezi kupata fursa sahihi hivyo niwaombe sana muwe wepesi katika kutafuta taarifa ili mnufaike na fursa za uwezeshaji zinazotolewa na Serikali" alisema Magesa.

Akizungumzia suala la mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri nchini, Magesa alisema mikopo hiyo haiombwi kwa maandiko mradi yaliyopo kwenye makaratasi bali inaombwa kwenye mfumo na majibu yanapatika kwenye mfumo hivyo amewasihi vijana kufuata maelekezo na utaratibu ili wapate mikopo na fursa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Power of Youth Development (PYD), Pedius Boniphace alisema waliandaa warsha hiyo ili vijana zaidi ya 40 kutoka mashirika mbalimbali waweze kukutana na taasisi zinazosimamia na kutekeleza fursa za kisera za vijana ili wajadili fursa za kiuchumi zinazopatikana hususani mitaji.

Alieleza kuwa warsha hiyo imefanyika ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi ambao unatekelezwa na UNDP kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana ambao unaitwa 'Dumisha amani'.

"Huu ni mradi unaotekelezwa kwa ajili ya kuwawezesha vijana kuendelea kudumisha amani" alisema Boniphace.

Alisema walikutana na vijana hao miezi mitano iliyopita, wakazungumza nao ambapo wengi wao walionesha kutokuwa na imani na taasisi za umma zinazosimamia fursa zao.

Baada ya kuona vijana hawana imani wakaona wawakutanishe na viongozi wanaosimamia hizo fursa ili wawaeleze vijana namna bora ya kuweza kufanya na hatimaye wazifikie fursa zinazowezeshwa na Serikali.

Aidha alisema Serikali inapaswa iwe inatoa taarifa kuanzia ngazi ya Mtaa hatua itakayosaidia kupunguza malalamiko ya vijana ya kutofikiwa na fursa wanazozitoa pamoja na kuongeza bajeti kwani vikundi vinavyohitaji fedha za mikopo ni vingi.

Naye Afisa Uchunguzi kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza, Magesa Cosmas alitoa wito kwa viongozi wanaohusika na utoaji wa mikopo kuhakikisha wanafuata sheria, kanuni na taratibu zilizoweka katika utoaji wa mikopo hiyo ili waweze kujiepusha na rushwa.
Akizungumza kwa niaba ya vijana walioshiriki kwenye warsha hiyo, Paul Kashilimu alisema wamekuwa wakikosa fursa mbalimbali kutokana na kukosa uelewa na kukosa mtandao wa wahusika wanaosimamia fursa zinazotangazwa.

Alisema warsha hiyo imekuwa chachu kwa vijana kuongeza jitihada katika kutafuta taarifa sahihi huku akiwapongeza viongozi wanaosimamia fursa zao kwa namna walivyo wapa mwanga mzuri wakuzifikia fursa.

Awali akizungumza kwenye warsha hiyo, Katibu Tawala Wilaya ya Nyamagana ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya uhakiki wa fedha za mikopo zinazotolewa na Halmashauri, Thomas Salala aliwasisitiza vijana kuziheshimu na kuziogopa fedha za mikopo.

"Mnapochukua fedha hizi za mikopo hakikisheni mnazifanyia kazi ipasavyo na, lakini mkizibadilishia matumizi kwa tamaa hamtaweza kufanikiwa na mtashindwa kurejesha fedha hivyo kuweni na nidhamu kwenye suala la fedha" alisema Salala.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Nyamagana Thomas Salala.
Afisa Maendeleo ya Vijana Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Michael Magesa.
Mkurugenzi wa Shirika la Power of Youth Development (PYD), Pedius Boniphace.
Viongozi na vijana mbalimbali wakiwa kwenye picha ya pamoja.
Viongozi na vijana mbalimbali wakiwa kwenye picha ya pamoja.
Na Hellen Mtereko, Mwanza.

No comments:

Powered by Blogger.