LIVE STREAM ADS

Header Ads

UPANUZI KITUO CHA AFYA KASUNGAMILE SENGEREMA WAFIKIA ASILIMIA 90

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Wakazi wa Kata ya Kasungamile na maeneo jirani katika Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, wanatarajia kuanza kunufaika na huduma za afya karibu baada ya upanuzi wa Zahanati ya Kasungamile kuwa Kituo cha Afya kukamilika.

Akizungumzia upanuzi huo ambao umefikia asilimia 90, Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Kasungamile, Dkt. Ibrahim Mwalisatile alisema mwaka 2025/26 Zahanati hiyo ilipokea fedha kutoka serikalini ili kufanyiwa upanuzi kuwa Kituo cha Afya kwa lengo la kuboresha zaidi huduma za afya.

Mwalisatile alieleza kuwa upanuzi wa kituo hicho utakapokamilika utahudumia takribani wateja 100,00 ambapo awali kikiwa Zahanati uwezo ni kuhudumia wateja 3,600 hadi 4,000.

Aidha aliiomba Serikali kuwaongezea bajeti kwa ajili ya kuongeza jengo la mionzi, kulaza wagonjwa, kuhifadhia maiti pamoja na nyumba za watumishi.

"Tukiongeza majengo hayo, wagonjwa watapa huduma kirahisi kwa sababu hapa ni ngumu ikitokea mtu amekuja kutibiwa akiwa amevunjika inabidi aende Sengerema akapige 'x-ray' ndipo arudi kwa ajili ya matibabu" alisema Mwalisatile.

Kwa upande wake Msimamizi wa mradi huo kutoka Idara ya Miundo Mbinu, Maendeleo ya Mjini na Vijijini Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Mhandisi Gilbert Maro alisema mradi huo uliogharimu milioni 683 umefikia asilimia 90 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba 30, 2026.

Naye Dorcas Paul ambaye ni mkazi wa Sengerema aliomba mradi huo ukamilike kwa wakati ili waweze kupata huduma kwa urahisi na waepukane na mwendo mrefu wa kwenda kuifuata huduma hiyo mbali.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kasungamile, Godfrey Joseph alisema ukosefu wa kituo cha afya ilikuwa adha kubwa kwa wakazi wa eneo hilo kutokana na kuwa mbali na huduma za afya.

Mradi huo ulianza kutekelezwa Mei 18, 2026 na unatarajia kuhudumia Vitongoji sita ambavyo ni Kasungamile, Ilekanyiro, Nyantakubwa, Nyamililo na Nyachina.
Na Chausiku Said, Mwanza

No comments:

Powered by Blogger.