LIVE STREAM ADS

Header Ads

MIAKA 60 YA USHIRIKIANO WA MWANZA, WÜRZBURG KUFUNGUA FURSA ZAIDI

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Ushirikiano wa Jiji la Mwanza (Tanzania) na Jiji la Würzburg (Ujerumani), unatarajia kufungua fursa zaidi baada ya kufikisha miaka 60 tangu uasisiwe.

Ushirikiano huo unatarajiwa kuleta manufaa zaidi katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, uwekezaji, elimu, afya, teknolojia na uwezeshaji wanawake na vijana.

Ushirikiano huo unalenga kuhakikisha kuwa urafiki uliojengwa kwa kipindi cha miongo sita unazidi kuleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi wa majiji hayo kupitia fursa za kiuchumi, kubadilishana maarifa na uzoefu katika sekta mbalimbali.

Akizungumza jijini Mwanza Jumatatu Novemba 09, 2026, katika maadhimisho ya miaka 60 ya urafiki na ushirikiano wa majiji hayo, Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Constantine alisema ni muhimu kuendeleza mahusiano hayo kwa kuwashirikisha wananchi katika makundi mbalimbali.

Alisema ushirikiano huo uliojengwa kwa muda mrefu kupitia juhudi za watu wa pande zote mbili unapaswa kuendelea kukua kwa kuwafikia wanawake, vijana, wafanyabiashara na makundi mengine ya kijamii ili kila upande uweze kunufaika.

Naye Meya wa Jiji la Würzburg, Martini Heilig alisisitiza umuhimu wa kuendeleza uhusiano huo wa kihistoria na kufungua milango ya ushirikiano mpya katika sekta mbalimbali kwa manufaa ya wananchi wa majiji hayo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Jubilate Lawuo, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, CP Salum Hamduni, alisema ni wakati sasa wa kutumia urafiki huo wa kihistoria kufungua fursa mpya za kiuchumi na uwekezaji kwa kuunganisha Mwanza na wafanyabiashara, taasisi za uwekezaji, vyuo vikuu na vyama vya wataalamu kutoka Würzburg.

Lawuo alisema majiji hayo yana nafasi kubwa ya kupanua ushirikiano katika elimu ya ufundi stadi, uhamishaji wa teknolojia, ujasiriamali, uwezeshaji wa vijana pamoja na kuongeza ushiriki wa wanawake katika shughuli za kiuchumi.

“Dhamira yetu inapaswa kuwa kubadilisha miaka 60 ya urafiki kuwa enzi mpya ya ustawi wa kiuchumi wa pamoja” alisema.

Katika sekta ya afya, ushirikiano huo umechangia kuimarisha huduma kupitia Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando pamoja na Kituo cha Else Kröner (Else Kröner Center Würzburg-Mwanza), kilichoanzishwa mwaka 2020.

Kwa upande wa elimu, ushirikiano huo umeendelea kutoa manufaa kwa taasisi mbalimbali, ambapo Mwalimu Roseline Kitoka wa Shule ya Msingi Butimba ni miongoni mwa wanufaika wa miradi inayotekelezwa kwa ushirikiano na wadau kutoka Jiji la Würzburg, akieleza kuwa miradi hiyo imechangia kuboresha mazingira na huduma za elimu.

Urafiki kati ya Mwanza na Würzburg ulianzishwa Juni 28, 1966 na kwa kipindi cha miaka 60 umekuwa daraja la kubadilishana maarifa, uzoefu na fursa za maendeleo katika sekta za afya, elimu, mazingira, utamaduni na utawala bora.
Na Chausiku Said, Mwanza
Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza, Sima Costantine.
Meya Jiji la Mwanza, Sima Costantine (kulia), akiteta jambo na Meya wa Jiji la Würzburg, Martini Heilig (kushoto).
Meya Jiji la Mwanza, Sima Costantine (kulia), akimkabidhi zawadi Meya wa Jiji la Würzburg, Martini Heilig (kushoto).
Viongozi mbalimbali akiwemo Naibu Meya Jiji la Mwanza (kushoto), wakifuatilia maadhimisho hayo.
Wananchi na viongozi mbalimbali wakifuatilia maadhimisho hayo.

No comments:

Powered by Blogger.