USHIRIKIANO WA SERIKALI NA WORLD VISION WAIMARISHA AFUA ZA LISHE SHINYANGA
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Serikali kwa kushirikiana na Shirika la World Vision Tanzania imeendelea kuimarisha afua za lishe na afya ya uzazi katika Mkoa wa Shinyanga kupitia utekelezaji wa mradi wa Grow ENRICH unaotekelezwa katika Halmashauri ya Shinyanga Mjini na Kishapu.
Hayo yalibainishwa Jumatatu Januari 26, 2026 jijini Mwanza katika jukwaa la wadau wa maendeleo lililolenga kujifunza kupitia mradi wa Grow ENRICH namna ambavyo umesaidia kupunguza utapiamlo na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu lishe bora.
Mtaalam wa Lishe kutoka Wizara ya Afya, Grace Mushi alisema mradi wa Grow ENRICH unaofadhiliwa na World Vision Tanzania unatekeleza shughuli mbalimbali za afya pamoja na lishe na Serikali ya Jamahuri ya Muungano wa Tanzania inatekeleza mpango kazi jumuishi wa masuala ya lishe kwa mwaka 2021/22 hadi 2025/26.
Mushi alieleza kuwa Tanzania inakabiliwa na matatizo makuu matatu ya lishe ikiwa ni pamoja na utapiamlo, lishe pungufu na lishe kuzidi ambapo alibainisha kuwa kwa watoto, udumavu uko asilimia 30, uzito pungufu asilimia 12 na utapiamlo ukondefu asilimia tatu.
Kwa upande mwingine alifafanua kuwa upungufu wa madini na vitamini unawapata watoto na wanawake ambapo asilimia 59 ya watoto na asilimia 42 ya wanawake wa umri wa kuzaa wana upungufu wa damu, na utapilomlo wa lishe ya kuzidi unashika kasi ambapo wanawake ni asilimia 36 na asilimia nne ya watoto wana uzito uliozidi.
"Serikali kwa kushirikiana na wadau imefanya mambo mengi, ikiwemo kutoa matone ya vitamini A kwa watoto, kutoa elimu kwa wananchi kupitia vituo vya afya na jamii, na kufanya urutubishaji wa chakula kwa kuongeza madini na vitamini kwenye vyakula" alisema Mushi.
Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Kaimu Afisa Lishe wa Mkoa wa Shinyanga, Mussa Makungu alisema mradi wa Grow ENRICH unatekelezwa katika Kata sita na Vijiji 29 katika Halmashauri ya Shinyanga DC, huku Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu ukitekelezwa katika Kata tatu na Vijiji 12.
Makungu alisema mradi huo umechangia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi pamoja na kuondoa mila potofu zilizokuwa zinaathiri hali ya lishe kwa watoto, hasa katika maeneo ya vijijini.
"Kumekuwa na mabadiliko chanya katika ushiriki wa wanaume kwenye masuala ya lishe ngazi ya familia, hali iliyokuwa changamoto kubwa awali, kupitia World Vision, vikundi vya kijamii viliundwa kwa lengo la kutoa elimu ya lishe, kuwahamasisha mama wajawazito kuwahi kliniki pamoja na kutambua dalili hatarishi kabla ya changamoto kutokea" alisema Makungu.
Kwa upande wake Mratibu wa Sekta ya Afya na Lishe kutoka Shirika la World Vision Tanzania, Dkt. Stanford Kaserwa alisema mradi umefikia takribani watu laki moja (123,000) sawa na asilimia 91 ya walengwa, shule 55 zimefikiwa katika masuala ya vyakula vilivyoimarishwa kwa virutubishi, pamoja na Kaya zaidi ya 400.
Naye Mkurugenzi Mtendaji Shirika la KIVULINI, Yasin Ally alisema kwa mujibu wa takwimu za Taasisi ya Takwimu ya Taifa, kiwango cha utapiamlo katika Mkoa wa Shinyanga kilikuwa asilimia 30, lakini kupitia mchango wa World Vision, Kivulini na wadau wengine, kiwango hicho kimeshuka hadi asilimia 27.




No comments: