LIVE STREAM ADS

Header Ads

BODI YA UTALII TANZANIA (TTB) KANDA YA ZIWA YATOA ELIMU KWA WANAFUNZI WA SAUT MWANZA

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Kanda ya Ziwa imeendelea kutembelea taasisi mbalimbali za elimu, kwa lengo la kutoa elimu ya utalii na kuhamasisha waalimu na wanafunzi katika taasisi hizo kutembelea vivutio vya utalii nchini.

Mkuu Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Kanda ya Ziwa, Rhoda Kabarua amesema mkakati huo unahusisha shule za msingi, sekondari na vyuo ambapo wanafunzi wanapata fursa ya kufahamu vivutio vya utalii nchini na hivyo kuongeza hamasa ya kukuza utalii wa ndani.

Kabarua ameyasema hayo Ijumaa Februari 20, 2026 baada ya kutoa elimu kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaosoma masomo ya utalii na ukarimu katika Chuo Kikuu cha SAUT jijini Mwanza.

"Tunambelea taasisi mbalimbali za elimu kukutana na waalimu pamoja na wanafunzi ili kuwaelimisha kuhusu vivutio vinavyopatikana kwenye maeneo yetu na namna ya kupanga safari ya kutembelea vivutio hivyo" amesema Kabarua. 

Kabarua pia ameipongea Idara ya Utalii na Ukarimu ya Chuo Kikuu cha SAUT jijini Mwanza kwa kuanzisha Makumbusho ya Chuo hicho iliyosheheni taarifa na kumbukumbu mbalimbali hatua ambayo itasaidia kupanua wigo wa sekta ya utalii.

Katika hatua nyingine Kabarua ameongeza kuwa katika kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Bodi ya Utalii Kanda ya Ziwa imeandaa safari ya utalii siku ya jumamosi tarehe 07 Machi 2026 kwa wananchi kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii ikiwemo Hifadhi ya Taifa Serengeti, Kisiwa cha Saanane na Rubondo na hivyo kuwahamasisha kushiriki safari hiyo ili kufurahia utalii wa ndani kwa gharama nafuu.

Nao wanafunzi wa utalii Chuo Kikuu SAUT akiwemo Anna Singo na Ezekiel Galiwene wamesema hatua ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Kanda ya Ziwa kutembelea taasisi za elimu inasaidia wanafunzi kufahamu shughuli za bodi hiyo, vivutio vya utalii na kuongeza hamasa ya utalii wa ndani.

Naye Mkuu wa Idara ya Utalii na Ukarimu Chuo Kikuu SAUT, Magdalena Ngassa amesema ushirikiano baina ya Idara hiyo na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Kanda ya Ziwa, unasaidia wanafunzi kufahamu vivutio vya utalii huku wakipata mafunzo kwa vitendo na hivyo kuwa bora baada ya kuhitimu masomo.
Na George Binagi, Mwanza
Mkuu Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Kanda ya Ziwa, Rhoda Kabarua akiwasilisha mada kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wanaosoma masomo ya utalii katika Chuo Kikuu cha SAUT jijini Mwanza kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu vivutio vya utalii na kuwahamasisha kutembelea vivutio hivyo.
Mmoja wa wanafunzi wa Chuo Kikuu SAUT jijini Mwanza akiuliza swali wakati Mkuu Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Kanda ya Ziwa, Rhoda Kabarua akiwasilisha mada kuhusu vivutio vya utalii nchini na namna ya kuvikia.
Maafisa wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), wakiongozwa na Mkuu wa Kanda ya Ziwa, Rhoda Kabarua (wa pili kulia) wakikabidhi machapisho mbalimbali ya utalii kwa ajili ya wanafunzi wa Chuo Kikuu SAUT jijini Mwanza wanaosoma masomo ya utalii.
Mkuu wa Idara ya Utalii na Ukarimu Chuo Kikuu cha SAUT jijini Mwanza, Magdalena Ngassa (katikati), akimuongoza Mkuu Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Kanda ya Ziwa, Rhoda Kabarua (kushoto) kuelekea kwenye Makumbusho ya Chuo hicho yenye historia na kumbukumbu mbalimbali. Kulia ni Rais wa Umoja wa Wanafunzi wa Utalii SAUT, Ezekiel Galiwene.
Mkuu Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Kanda ya Ziwa, Rhoda Kabarua (katikati mbele) akitembezwa na Kiongozi wa Makumbusho ya SAUT, Michael Masala kutembelea Makumbusho hiyo. Wengine ni Maafisa wa TTB Kanda ya Ziwa na wanafunzi wa utalii na ukarimu SAUT jijini Mwanza.
Mkuu Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Kanda ya Ziwa, Rhoda Kabarua (wa tano kutoka kushoto) akiwa kwenye picha ya pamoja na maafisa wa TTB, wanafunzi wa masomo ya utalii SAUT na Mkuu wa Idara ya Utalii na Ukarimu SAUT, Magdalena Ngassa (mwenye nguo nyeupe katikati).
Maafisa wa TTB wakiongozwa na Mkuu Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Kanda ya Ziwa, Rhoda Kabarua wakipata maelezo mbalimbali kuhusu Makumbusho ya SAUT ambayo ina muda wa miaka miwili tangu ianzishwe kwa lengo la kutunza kumbumbuku mbalimbali za chuo hicho huku pia ikitumika kwa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wa chuo hicho.
Mkuu Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Kanda ya Ziwa, Rhoda Kabarua (katikati) akizungumza na wanafunzi wa masomo ya utalii Chuo Kikuu cha SAUT baada ya kutembelea Makumbusho ya Chuo hicho.
Mwonekano wa baadhi ya majengo katika Chuo Kikuu cha SAUT jijini Mwanza.

No comments:

Powered by Blogger.