MWANZA: WANAHABARI, WANAFUNZI SAUT WANOLEWA KUANDIKA HABARI ZA TIJA, KULINDA ZIWA VICTORIA
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Shirika lisilo la kiserikali la Synergistic Globe imetoa mafunzo kwa wanahabari na wanafunzi uandishi wa habari kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) jijini Mwanza, kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kuandika habari za mazingira zenye tija hususani katika uchafuzi wa plastiki ndani ya Ziwa Victoria.
Mafunzo hayo yamefanyika Jumamosi Machi 14, 2026 yakilenga kuwasaidia wanahabari kuibua na kuandika habari zinazogusa changamoto za mazingira, hususan uchafuzi wa taka za plastiki katika Ziwa Victoria, ambalo ni chanzo kikuu cha maisha kwa mamilioni ya wananchi katika Ukanda wa Afrika Mashariki.
Aidha mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Marafiki wa Ziwa Victoria unaofadhiliwa na Global Greengrants Fund, ukilenga kupunguza athari za taka za plastiki na kuhamasisha jamii kulinda vyanzo vya maji.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Shirika hilo Vitus Medard amesema baada ya mafunzo, washiriki watapewa fursa ya kuandaa makala bunifu za habari za mazingira zitakazosaidia kuongeza uelewa wa jamii kuhusu athari za taka za plastiki katika Ziwa Victoria.
Aidha amesema tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa uchafuzi wa plastiki tayari umeanza kuathiri viumbe hai ndani ya ziwa hilo. Utafiti uliofanyika mwaka 2015 katika eneo la Mwanza ulibaini kuwa chembechembe ndogo za plastiki (microplastics) zilipatikana katika takribani asilimia 20 ya samaki aina ya sangara na sato waliopimwa.
Amesema jambo linaloonyesha kuwa plastiki imeanza kuingia katika mfumo wa chakula cha binadamu kupitia samaki wanaovuliwa ziwani humo.
Aidha tafiti nyingine zimeonesha kuwa maji ya Ziwa Victoria yana maelfu ya chembechembe za plastiki katika kila kilomita ya mraba, nyingi zikiwa na ukubwa wa chini ya milimita moja ambazo ni rahisi kumezwa na samaki na viumbe wengine wa majini.
Kadhalika naye Mratibu Mtendaji wa Shirika hilo Angelina Manyama (PdD Candidate) na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT) amesema, taka za plastiki pia zimekuwa chanzo cha changamoto nyingine za mazingira mijini.
Amesema miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na kuziba kwa mifereji ya maji. Alitolea mfano mafuriko yaliyotokea hivi karibuni katika eneo la Mkuyuni jijini Mwanza, ambapo mkusanyiko wa taka za plastiki kwenye mitaro unatajwa kuwa moja ya sababu zinazochangia maji kushindwa kupita kwa urahisi wakati wa mvua kubwa.
Kutokana na hali hiyo, taasisi hiyo kupitia mradi wa Marafiki wa Ziwa Victoria inahamasisha suluhisho endelevu ikiwa ni pamoja na ukusanyaji na urejelezaji wa taka za plastiki, huku ikisisitiza kuwa plastiki pia inaweza kuwa fursa ya kiuchumi kwa jamii.
Ameongeza kuwa kupitia ushiriki wa wanahabari, jamii inaweza kupata taarifa sahihi kuhusu madhara ya plastiki, lakini pia kufahamu fursa zinazoweza kupatikana kupitia uchumi wa urejelezaji.
Mada mbalimbali habari za uchunguzi na uandishi wa habari wenye suluhisho, zimewasilishwa na wataalam wa habari na mazingira akiwemo Dkt. Peter Mataba (PhD) na Dkt.Pascal Shao (PhD) ambao pia ni Wahadhiri Chuo Kikuu SAUT.
Na George Binagi, BMG
Wanahabari walioshiriki mafunzo hayo ni kutoka BMG Media, Azam Media, Sahara Media na IPP Media. Pia wanafunzi wameshiriki wanafunzi wa SAUT wa masomo ya uandishi wa habari na mawasiliano ya umma.


No comments: