LIVE STREAM ADS

Header Ads

VIKUNDI 12 VYA WANAWAKE VYAZINDUA VIWANDA VIDOGO KAHUMULO SENGEREMA

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Meneja Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Mwanza, Bakari Songwe akikata utepe kuashiria uzinduzi wa viwanda mbalimbali vilivyoanzishwa na vikundi 12 vya wanawake katika Kijiji cha Kahumulo wilayani Sengerema.
***

Vikundi 12 vya wanawake katika Kijiji cha Kahumulo, Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, vimefanikiwa kuzindua viwanda vinne vidogo vya usindikaji wa mazao.

Viwanda hivyo ni pamoja na kituo cha uokaji mikate, usindikaji wa maziwa lishe, utengenezaji wa mvinyo na usindikaji wa viazi lishe. 

Mafanikio hayo yametokana na mafunzo na kujengewa uwezo na Shirika la MikonoYetu, linalotetea haki za wanawake na lenye makao yake jijini Mwanza.

Uzinduzi wa viwanda hivyo ulifanyika Jumatano Machi 04, 2026 ukiambatana na uzinduzi wa mradi wa ufugaji wa nyuki na uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha Msichana Tai Kahumulo. 

Kituo hicho kinatarajiwa kutoa mafunzo mbalimbali ya stadi za maisha kwa wasichana ikiwemo ushonaji nguo, utengenezaji wa taulo za kike zinazoweza kutumika zaidi ya mara moja pamoja na kazi nyingine za mikono.

Mmoja wa wanachama wa umoja huo, Jenipher Hokololo alisema baada ya kupatiwa mafunzo ya uokaji mikate na Shirika la MikonoYetu, wamefanikiwa kuboresha uzalishaji wao. 

Hata hivyo Hokololo alibainisha kuwa bado wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa masoko makubwa zaidi.

"Soko bado halijawa zuri sana. Kwa sasa tunauza hapa hapa kijijini na katika maeneo ya jirani kama vile Lubanda, Nyampande na Nyeitundu. Tunaomba kupata ufadhili zaidi ili kutusaidia kupanua soko letu" alisema Hokololo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la MikonoYetu, Esther Masawe alisema hadi sasa Umoja wa Wanawake Kahumulo una zaidi ya wanachama 300, ambao wamepatiwa mafunzo mbalimbali yaliyowawezesha kuanzisha viwanda hivyo vidogo, hatua iliyowasaidia kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao.

Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Mwanza, Bakari Songwe aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ya Siku ya Wanawake Duniani, aliwapongeza wanawake hao kwa juhudi na mafanikio yao.

Aliwahimiza kuongeza bidii katika uzalishaji ili kuendelea kupanua wigo wa masoko yao na kuwa mfano bora kwa wanawake wengine ndani na nje ya Kijiji cha Kahumulo.

Hafla ya uzinduzi wa viwanda hivyo pamoja na uwekaji wa jiwe la msingi la Kituo cha Msichana Tai Kahumulo ilifanyika sambamba na shamrashamra za Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yenye kaulimbiu isemayo:
"Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana: Msingi Jumuishi wa Kufikia Dira ya Maendeleo 2050".

Maadhimisho hayo yalifikia kilele chake duniani kote Jumapili Machi 08, 2026, yakisisitiza umuhimu wa wanawake na wasichana katika kujenga jamii jumuishi, imara na yenye maendeleo endelevu.
Na Mariam Ngollo, Mwanza
Meneja Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Mwanza, Bakari Songwe akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika Kijiji cha Kahumulo wilayani Sengerema.
Jengo la kiwanda kidogo cha wanawake Kahumulo kwa ajili ya usindikaji viazi lishe.
Mradi wa ufugaji nyuki Kahumulo.
Meneja Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Mwanza, Bakari Songwe (katikati) akiwa na viongozi kutoka shirika la Mikono Yetu.
Mmoja wa wanawake wajasiriamali Kijiji cha Kahumulo wilayani Sengerema akitoa shukurani kwa Shirika la Mikono Yetu baada ya kuwajengea uwezo na kuanzisha miradi mbalimbali ya ujasiriamali kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.
Wananchi wakifuatilia maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika Kijiji cha Kahumulo wilayani Sengerema, yakiambatana na uzinduzi wa viwanda vidogo vilivyoanzishwa na vikundi 12 vya wanawake pamoja na uwekaji jiwe la msingi Kituo cha Msichana Tai Kahumulo, Sengerema.
Tazama Video hapa chini

No comments:

Powered by Blogger.