PROF. SHEMDOE AWATAKA WAKUU WA MIKOA KUSIMAMIA HALMASHAURI ZIWE NA MIPANGO MADHUBUTI YA KUZALISHA NAFAKA NA MAZAO
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com








Na OWM – TAMISEMI, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amewataka Wakuu wa Mikoa nchini kuhakikisha Halmashauri zinaweka mipango madhubuti ya kuendeleza uzalishaji wa nafaka na mazao mchanganyiko kwa kuzingatia kanuni za kilimo bora.
Prof. Shemdoe ametoa wito huo leo Aprili 16, 2026 wakati akifunga kikao cha Wizara ya Kilimo na Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI cha wasilisho la tathmini ya utekelezaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), kilichohudhuriwa na Wakuu wa Mikoa, Makatibu Tawala wa Mikoa, Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Washirika wa maendeleo na Wadau mbalimbali wa Sekta ya kilimo.
“Tutakapozingatia kanuni bora za kilimo, tutapata mazao ambayo yakipelekwa katika soko la nje yatauzwa kwa bei nzuri zitakazowanufaisha wakulima wa kitanzania,” amesisitiza Prof. Shemdoe.
Aidha, Prof. Shemdoe amewataka Wakuu wa Mikoa hao kusimamia kikamilifu ukusanyaji na matumizi sahihi ya mapato ya ndani yatokanayo na mazao ya kilimo ili kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo na biashara ya mazao nchini, ikizingatiwa kwamba zaidi ya asilimia 75 za halmashauri nchini zinategemea mapato ya ndani kutoka kwenye kilimo.
“Katika Mwaka wa Fedha 2026/27 tunategemea kukusanya zaidi ya trilioni 2, na chanzo kikubwa kinachotegemewa ni mazao mchanganyiko hivyo Wakuu wa Mikoa hamna budi kuongeza nguvu katika uzalishaji ili tufikie lengo la makusanyo,” Prof. Shemdoe amehimiza.
Akizungumzia suala la ushirikiano wa Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI na Wizara za Kisekta, Prof. Shemdoe amemshukuru na kumpongeza Waziri wa Kilimo Mhe. Daniel Chongolo kwa kuona umuhimu wa kushirikiana na OWM-TAMISEMI ambayo inaratibu na kusimamia shughuli zote zinazowagusa wananchi moja kwa moja kupitia Sekreterieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.







No comments: