BILIONI 127 KUTEKELEZA MIRADI YA UMEME VIJIJINI MKOANI MWANZA
Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema Serikali kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA), inatekeleza miradi yenye thamani ya Tsh. Bilioni 127.7 ili kufikisha huduma ya umeme kwenye vijiji na vitongoji vyote pamoja wa majiko ya nishati safi ya kupikia.
Mtanda ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha kwanza cha Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na wabia wa maendeleo ya nishati (Energy Development Partner- EDPG) kilichofanyika jijini Mwanza.
Mtanda amesema miradi inayotekeleza mkoani Mwanza ni pamoja na uwekaji wa miundombinu ya nishati safi ya kupikia kwenye magereza na usambazaji wa umeme jua visiwani.
Ameongeza kuwa hadi kufikia mwezi Aprili 2026 vitongoji 1,597 kati ya 3,448 sawa na 46% vimefikiwa na nishati ya umeme na kwamba wakandarasi wameshapewa zabuni ya kufikisha huduma hiyo katika maeneo ambayo bado.
Mtanda amesema kuna vijiji 24 ambavyo bado havijafikiwa na nishati ya umeme mkoani Mwanza huku vijiji 522 vikiwa vimefikiwa na nishati hiyo hatua ambayo itasaidia wananchi kutumia nishati ya umeme kujikwamua kiuchumi.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Balozi Meja Jenerali (Mstaafu), Jacob Kingu amesema bodi hiyo imejipanga kuhakikisha inatekeleza kwa ufanisi miradi inayofadhiliwa na Serikali pamoja na wabia wa maendeleo.
TAZAMA VIDEO HAPA CHINI

No comments: