LIVE STREAM ADS

Header Ads

SEKTA YA SHERIA KUWA KICHOCHEO CHA UKUAJI UCHUMI

Yaliyomo humu (Habari, Matangazo na Maoni) si msimamo wa BMG Media. Mawasiliano +255 757 432 694 ama ripotabmg@gmail.com
Wizara ya Katiba na Sheria imejipanga kuibadilisha Sekta ya Sheria kutoka kuwa sekta ya huduma na kuwa kichocheo cha ukuaji wa uchumi na uwekezaji nchini.

Haya yamebainishwa Bungeni jijini Dodoma, leo 24 Aprili 2026, na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt Juma Zuberi Homera, wakati alipokuwa akiwasilisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

“Wizara itajikita katika falsafa mpya ya uendeshaji wa Sekta ya Sheria kutoka Mfumo wa Sekta ya Sheria Unaotumia Rasilimali Bila Kutoa Matokeo Yanayoonekana kwenda mfumo wa Sekta ya Sheria Unaohakikisha Haki inapatikana na Matokeo yanaonekana’’ Amesema Dkt. Homera.

Dkt. Homera pia amesema Wizara imejipanga kujenga Sekta ya Sheria inayotoa haki kwa wakati, yenye ufanisi mkubwa, inayotumia teknolojia, na inayochochea maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Aidha, Dkt Homera amesema wizara itafanya maboresho ya mifumo ya Sheria ili kuwezesha utekelezaji wa DIRA 2050 kwa kuweka mifumo ya kisheria imara, inayotabirika na kuchochea uwekezaji pamoja na kulinda rasilimali za Taifa.

‘’Sekta ya Sheria inachukua nafasi mpya katika historia ya Taifa letu, sio tena kama msimamizi wa sheria pekee, bali kama injini ya uthabiti wa Taifa na kichocheo cha maendeleo ya Uchumi katika kufikia malengo ya DIRA 20250’’ amesema Dkt. Homera.

Wizara pia imejipanga kuimarisha mifumo ya kidijitali katika sekta ya Sheria kwa kujenga, kuboresha na kuunganisha mifumo ya TEHAMA kwa lengo la kurahisisha upatikanaji haki kwa wananchi na taarifa katika Sekta ya Sheria nchini ili kuchangia hatua za kufikia malengo ya DIRA 2050.

No comments:

Powered by Blogger.